Balozi wa China katika Umoja wa Afrika AU
amekanusha vikali madai ya vyombo vya habari vya Magharibi vilivyodai
kuwa nchi hiyo inafanya ujasusi katika Makao Makuu ya AU mjini Addis
Ababa, Ethiopia.
Kuang Weilin amesema kuwa madai ya
gazeti la Ufaransa la Le Monde ya kwamba nchi yake inafanya ujasusi
katika Makao Makuu ya AU mjini Addis Ababa tangu mwaka 2012 hadi 2017 ni
ya kipuuzi na hayana ukweli wowote.
Balozi huyo wa China amesema hayo
pambizoni mwa kikao cha wakuu wa Umoja wa Afrika kilichofanyika Jumapili
na Jumatatu tarehe 28 na 29 Januari 2018 katika mji mkuu wa Ethiopia,
Addis Ababa.
Amesema: "Gazeti hilo la Ufaransa
limepoteza heshima yake kwa kusambaza madai hayo ya uongo siku ya Ijumaa
na kamwe madai kama hayo hayawezi kuharibu uhusiano wa China na
Afrika."
Siku ya Ijumaa gazeti la Le Monde la
Ufaransa lilinukuu baadhi ya duru za Umoja wa Afrika zikidai kwamba
wataalamu wa kompyuta wamegundua kuwa, kwa muda wa mwaka mzima sasa
taarifa za watumizi wa kompyuta wa AU zinapelekwa kwa upande wa tatu
ulioko mjini Shanghai, China.
Kwa upande wake, Umoja wa Afrika umesema
unashughulishwa zaidi na uhusiano imara kati ya Afrika na China kuliko
madai hayo ya gazeti la Ufaransa.
Itakumbukwa kuwa China ndiye mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa nchi za Afrika.
No comments:
Post a Comment