Rais wa Uganda atafakari kurejesha hukumu ya kifo
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema
anatafakari kurejesha hukumu ya kifo nchini humo ili kukabiliana na
wimbi kubwa la uhalifu nchini.
Katika
ujumbe aliotuma katika akaunti yake ya Twitter, Rais Museveni amesema
amekuwa akisita kutia saini kila hukumu ya kifo anayoletewa tokea mwaka
1999. Hukumu ya kifo ambayo ndio adhabu kali zaidi Uganda kwa
wanaohusika na uhalifu kama vile mauaji, uhaini na kunajisi haijawahi
kutekelezwa tangu mwaka 1999. Idara ya Magereza Uganda inasema hivi sasa
kuna wafungwa 278 ambao wamehukumiwa kifo lakini Rais Museveni hajatia
saini amri ya utekelezwaji wa hukumu hizo.
Rais
Museveni amesema watu wanatumia vibaya moyo wake wa huruma na sasa
wengine wanadhani wanaweza kutenda uhalifu bila kuadhibiwa. Amesema
anatafakari kuhusu kubadili msimamo wake huo wa kutotia siani adhabu ya
kifo.
Katika nchi jirani ya Kenya pia, hukumu ya kifo iko katika sheria
lakini marais wa nchi hiyo hawajatia saini amri ya utekelezwaji hukumu
hiyo kwa miaka 30 sasa. Oktoba mwaka 2016 Rais Uhuru Kenyatta alitia
saini amri ya kubatilisha hukumu ya kifo ya wanaume 2,655 na wanawake 92
na kuifanya iwe hukumu ya maisha jela. Wakosoaji wanasema kutotekelezwa
hukumu ya kifo kumepelekea kuongezeka kesi za uhalifu katika nchi hizo.
No comments:
Post a Comment