Friday, January 19, 2018

RAIA 700,000 WA SUDAN KUSINI WALIKIMBIA NJAA, VITA, MAGONJWA MWAKA JANA

Raia 700,000 wa Sudan Kusini walikimbia njaa, vita, magonjwa mwaka jana
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema raia takriabani laki 7 wa Sudan Kusini walikimbilia nchi jirani kutokana na migogoro, njaa na magonjwa katika mwaka 2017.
Ofisi hiyo imesema watu milioni 4 wamekimbia makwao, wakiwemo wakimbizi milioni 1.9 wa ndani, na zaidi ya milioni 2 waliokimbilia nchi za jirani zikiwemo Uganda, Kenya, Ethiopia, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ofisi hiyo pia imesema idadi ya Wasudan Kusini walioikimbia nchi yao mwaka jana, imepungua kuliko watu laki 7.6 mwaka juzi.
Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza mwezi Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.
Rais Salva Kiir (kushoto) na kiongozi wa waasi Riek Machar
Mwezi uliopita wa Disemba, Serikali ya Sudan Kusini ilitiliana saini mapatano ya usitishaji vita na makundi ya waasi nchini humo katika jitihada za hivi karibuni kabisa za kumaliza vita vya ndani ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa muda wa miaka minne nchini humo. Hata hivyo mapatano hayo yanalegalega huku kila upanda ukiutuhumu mwinginei kuwa unayakiuka.

No comments:

Post a Comment