Baada ya kuongezeka mashinikizo ya wananchi
na vyombo vya habari vya Marekani, rais wa nchi hiyo, Donald Trump
hatimaye amekubali kupimwa akili ili iweze kujulikana iwapo yuko salama
kiakili au la.
Gazeti la Daily Telegraph
limeripoti habari hiyo na kusema, baada ya Trump kukubali kupimwa akili,
zoezi hilo sasa litafanyika Ijumaa ijayo katika hospitali ya kijeshi
ya Walter Reed mjini Washington DC. Walter Reed ni hospitali kubwa zaidi
ya kijeshi nchini Marekani.
Imepangwa kuwa matokeo ya uchunguzi huo
wa akili ya Trump yatawekwa hadharani ili watu wote waweze kuyaona. Kwa
mujibu wa Telegraph, Trump amekubali kupimwa akili ili kupunguza wimbi
la uvumi ulioenea katika kila kona ya dunia kwamba rais huyo wa Marekani
hana akili timamu.
Suala la usalama wa kiakili wa Trump
limepata nguvu zaidi siku chache zilizopita baada ya kusambazwa kitabu
cha "Moto na Ghadhabu ndani ya White House ya Trump" kilichoandikwa na
mtunzi wa vitabu wa Kimarekani, Michael Wolff. Sehemu ya kwanza ya
maelezo ya kina ya kitabu hicho inayoakisi hofu na wasiwasi walionao
wasaidizi waandamizi katika Ikulu ya White House kuhusu uzima wa kiakili
wa rais wa Marekani ilichapishwa Jumatano iliyopita na gazeti la The
Guardian.
Katika sehemu moja ya kitabu hicho,
Michael Wolff anasimulia matukio ya kipindi cha mwaka mmoja wa urais wa
Donald Trump na kusema kuwa, rais huyo wa Marekani hata hawezi
kuwakumbuka marafiki zake wa zamani bali hata anasahau sana mambo
yaliyomtokea.
Vile vile kitabu hicho kinachora picha
inayoonesha udhalili wa rais wa Marekani Donald Trump na ukosefu wake
mkubwa wa heshima alioudhihirisha zaidi baada ya kuingia katika Ikulu ya
nchi hiyo. Kitabu hicho kinamuonesha Trump kuwa mtu mwenye fikra za
kitoto ambaye hakutarajia kabisa kushinda urais na kuingia katika Ikulu
ya White House.
No comments:
Post a Comment