Wakili wa mkuu wa zamani wa jeshi la Misri
ambaye ametangaza kuchuana na Rais Abdul Fattah el Sisi katika uchaguzi
ujao wa rais nchini humo amesema kuwa, mteja wake emepelekwa katika jela
ya kijeshi.
Habari hiyo imetangazwa leo na
gazeti la Ra'y al Yaum na kumnukuu Naser Amin, wakili wa Sami Hafez
Anan, mkuu wa zamani wa jeshi la Misri akiandika katika ukurasa wake wa
Facebook wamba ameruhusiwa kwenda kuonana na Anan katika jela ya
kijeshi.
Komandi Kuu ya vikosi vya ulinzi vya
Misri, Jumanne ilivyopita ilitoa tamko na kumlaumu Anan kwa kutangaza
kushiriki katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo. Aidha komandi hiyo
ilimtuhumu Anan kuwa amevunja sheria na kutoa maneno ya kichochezi dhidi
ya vikosi vya ulinzi vya Misri.
Tuhuma nyingine alizobebeshwa Sami Hafez
Anan baada ya kutangaza kuwa atachuana na Rais Abdul Fattah el Sisi
katika uchaguzi ujao ni pamoja na madai ya kughushi nyara na vyeti
rasmi.
Tayari Ahmad Shafiq, waziri mkuu wa zamani wa Misri ametangaza kujitoa katika kinyang'anyiro hicho.
Khaled Ali, mwanasiasa mwingine
aliyetangaza kuchuana na el Sisi naye ameshatangaza kujitoa katika
kinyang'anyiro hicho. Kwa hali hiyo, hivi sasa Rais wa Misri Abdul
Fattah el Sisi amebakia peke yake katika uchaguzi huo bila ya mpinzani
yeyote.
Uchaguzi wa Rais wa Misri unatarajiwa kufanyika kati ya tarehe 26 na 28 Machi mwaka huu wa 2018
No comments:
Post a Comment