Wednesday, January 24, 2018

LIBYA YAITUHUMU UTURUKI KUHUSIKA NA MIRIPUKO YA MABOMU ILIYOTOKEA BENGHAZI

Libya yaituhumu Uturuki kuhusika na miripuko ya mabomu iliyotokea Benghazi
Msemaji wa jeshi la taifa la Libya ameituhumu Uturuki kuwa imehusika na miripuko ya mabomu iliyotokea mjini Benghazi mashariki mwa Libya.
Hapo kabla pia Ahmad al-Mismari alikuwa ameituhumu serikali ya Ankara kuwa inaunga mkono ugaidi nchini Libya.
Watu wasiopungua 33 waliuawa na wengine 70 walijeruhiwa katika miripuko miwili ya mabomu iliyotokea mjini Benghazi usiku wa kuamkia jana.
Mripuko wa kwanza ulitokea mbele ya msikiti wa Baiatu-Ridhwan katika mtaa wa Al Salmani wakati waumini walipokuwa wanatoka msikitini humo wakati wa usiku. Mripuko wa pili ulitokea katika muda wa chini ya dakika 15 baadaye mbele ya Idara ya Uhamiaji mjini Benghazi.
Mji wa Benghazi unadhibitiwa na jeshi la taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar ambalo lilifanikiwa kuudhibiti kikamilifu mji huo wa mashariki mwa Libya tarehe 25 Desemba mwaka jana baada ya kuyatimua makundi yote ya wabeba silaha. 
Fayez al Sarraj (kushoto) na Jenerali Khalifa Haftar, viongozi wa mirengo mikuu hasimu nchini Libya
Amani na uthabiti vimetoweka nchini Libya tangu mwaka 2011 kutokana na uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na eneo kufuatia mapinduzi ya wananchi yaliyohitimisha utawala wa miongo kadhaa wa Muammar Gaddafi.
Kutokana na hitilafu zilizojitokeza kati ya vyama na makundi mbalimbali, kwa mwaka wa pili sasa Libya imekuwa na serikali mbili. Moja ni ile iliyo chini ya bunge la wawakilishi lenye makao yake katika mji wa Tobruk ulioko mashariki mwa nchi ambalo linaungwa mkono na jeshi la taifa linaloongozwa na Jenerali Haftar, na nyengine ni serikali ya umoja wa kitaifa yenye makao yake katika mji mkuu Tripoli ambayo inaongozwa na Fayez al-Sarraj na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Inafaa kuashiria kuwa nalo kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limeitumia fursa ya kukosekana amani na uthabiti wa kisiasa nchini Libya kujipenyeza katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.../ 

No comments:

Post a Comment