Walenga shabaha stadi wa jeshi la Yemen
wameua kwa kuwafyatulia risasi wanajeshi saba wa Saudi Arabia katika
maeneo ya Najran na Jizan, ikiwa ni radiamali kwa mashambulizi ya anga
ya Riyadh dhidi ya nchi hiyo.
Duru za kijeshi nchini Yemen zimesema walenga shabaha hao wa
jeshi la Yemen wakishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi
walifanya operesheni hiyo jana Ijumaa, ambao askari watano wa Saudia
waliuawa katika kijiji cha Hamezah katika eneo la Jizan, yapata kilomita
967 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Saudia, Riyadh.
Wanajeshi wengine wawili wa Saudia waliuawa jana alasiri kwa
kumiminiwa risasi katika kambi ya jeshi ya Raqabat al-Zour, iliyoko
katika eneo la Najran, umbali wa kilomita 844 kusini mwa Riyadh.
Mapema jana ndege za kivita za Saudia zilifanya mashambulizi matatu
ya anga katika wilaya ya Razih, kaskazini mashariki mwa eneo la Sa'ada.
Saudi Arabia na washirika wake waliivamia Yemen tangu mwezi Machi
mwaka 2015 na hadi sasa nchi hizo zinaendelea kuizingira nchi hiyo
kutokea nchi kavu, majini na angani na zimeua raia wasio na hatia zaidi
ya 13,000 na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
No comments:
Post a Comment