Katibu wa kamati ya utendaji ya Harakati ya
Ukombozi wa Palestina (PLO) amesema kuwa, hatua na vitendo vya Marekani
vimekuwa vikichochea vurugu na machafuko katika eneo la Mashariki ya
kati.
Saeb Erakat, amesema bayana
kwamba, hatua ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani
kuhusiana na Beitul-Muqaddas na wakimbizi wa Palestina ni ushahidi wa
wazi wa kuchochea na kueneza machafuko na vurugu katika eneo la
Mashariki ya Kati.
Afisa huyo mwandamizi wa Harakati ya
Ukombozi wa Palestina (PLO) amebainisha kwamba, uamuzi wa Trump wa
kuitambua Beitul Muqaddas kuwa eti ni mji mkuu wa utawala vamizi wa
Israel na kutaka uanzishwe mchakato wa kuhamishiwa ubalozi wa Washington
katika mji huo unaonyesha msimamo mkali, uenezaji vurugu na machafuko,
umwagaji damu na chokochoko alizo nazo rais huyo wa Marekani.
Saeb Erakat amesema, hatua hiyo ya Trump si chokochoko kwa Palestina tu bali kwa eneo zima la Mashariki ya Kati.
Katibu huyo wa kamati ya utendaji ya
Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesisitiza kuwa, njia pekee ya
kurejeshwa amani na utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati ni
kukomeshwa uvamizi wa Israel na kuimarishwa mamlaka ya kujitawala
Palestina mji mkuu wake ukiwa Beitul-Muqaddas.
No comments:
Post a Comment