Wednesday, January 24, 2018

RUSSIA NA SYRIA ZAKANUSHA MADAI YA MAREKANI KUHUSU SILAHA ZA KEMIKALI

Russia na Syria zakanusha madai ya Marekani kuhusu silaha za kemikali
Russia na Syria zimekadhibisha madai yaliyotolewa na Marekani na Ufaransa kwamba serikali ya Damascus imetumia silaha za kemikali katika mashambulizi yake, zikisisitiza kuwa tuhuma hizo zinapania kutia vizingiti katika juhudi za kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya amani mgogoro unaoshuhudiwa katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Taarifa ya serikali iliyopeperushwa na shirika rasmi la habari la Syria SANA imesema madai hayo ya US na Ufaransa ni urongo wa wazi ambao hauna lengo jingine ghairi ya kuvuruga mkondo wa kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa miaka kadhaa wa Syria.
Imeongeza kuwa, Syria ilikabidhi mrundiko wa silaha zake zote za kemikali mwaka 2014, kwa Umoja wa Mataifa na Shirika la Kupambana na Silaha za Kemikali OPCW, ambapo zote ziliharibiwa.
Makao Makuu ya Shirika la Kupambana na Silaha za Kemikali OPCW
Wakati huo huo, Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema katika mahojiano na shirika la habari la Interfax kwamba, Marekani inaeneza propaganada na ripoti ambazo hazijathibitishwa, ili kutia viunzi katika jitihada za Moscow za kutatuliwa mzozo wa Syria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson na mwenzake wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian siku ya Jumanne wakiwa mjini Paris walidai kuwa, Moscow inabeba dhima ya eti kutumiwa silaha za kemikali nchini Syria na eti kwamba wahusika wanapaswa kuwajibishwa na kuwekewa vikwazo.

No comments:

Post a Comment