Monday, January 29, 2018

NJAMA ZA RAIS EL-SISI ZA KUWA MGOMBEA PEKEE WA UCHAGUZI WA RAIS MISRI

Njama za Rais el-Sisi za kuwa mgombea pekee wa uchaguzi wa rais Misri
Nasser Amin, wakili wa Sami Hafez Anan, amesema kuwa, Anan anaendelea kushikiliwa katika jela nchini Misri.
Mkuu wa zamani wa majeshi ya Misri, Sami Hafez Anan hivi karibuni alitangaza azma yake ya kugombea katika uchaguzi ujao wa rais nchini humo lakini amepigwa kalamu na kuzuiwa kushiriki katika zoezi hilo. Anan si mtu wa kwanza kutiwa mbaroni na kuswekwa jela baada ya kutangaza azma yake ya kutaka kugombea kiti cha rais wa Misri. Kabla yake wanasiasa kama Ahmed Shafik, waziri mkuu wa zamani wa Misri na Khalid Ali, wakili na mwanasiasa mashuhuri wa nchi hiyo ama walitiwa jela au waliwekewa mashinikizo makali na kulazimika kutupilia mbali azma yao ya kugombea kiti cha rais wa Misri.
Sami Hafez Anan, aliyewahi kuwa mkuu wa majeshi nchini Misri ametiwa jela baada ya kutangaza azma ya kugombea nafasi ya rais
Katika uwanja huo, serikali ya Cairo ilimzulia kila mmoja wao sababu za kuwaweka jela au kuwekea mashinikizo. Kwa mfano tu mkuu wa zamani wa majeshi Misri yaani Sami Anan, yeye amewekwa jela kwa tuhuma za kukiuka sheria ikiwa ni pamoja na kutopata ridhaa ya jeshi kwa ajili ya kugombea katika uchaguzi wa rais, kughushi nyaraka rasmi na kadhalika kutoa matamshi ya kichochezi dhidi ya jeshi la nchi hiyo. Mienendo hiyo pamoja na mambo mengine, inatajwa na weledi wa mambo kwamba, ni sehemu ya mbinu zinazotumiwa na serikali ya Misri kuhakikisha uchaguzi ujao unafanyika kwa ushiriki wa mgombea mmoja ambaye ni Rais Abdel Fattah el-Sisi pekee, kama ilivyofanyika mwaka 2012 nchini Yemen, wakati Abdrabbuh Mansur Hadi alipokuwa mgombea pekee katika uchaguzi wa rais wa kimaonyesho.
Ahmed Shafik, waziri mkuu wa zamani wa Misri, ambaye naye alikumbwa na misukosuko baada ya kutanganza kugombea kiti cha rais
Ukweli ni kwamba uchaguzi unaopangwa kufanyika tarehe 26 na 28 mwezi Machi mwaka huu nchini Misri, sio uchaguzi huru na halisi, bali ni mchezo wa kutangaza utiifu mpya wa wananchi kwa Rais Abdel Fattah el-Sisi. Mienendo hiyo ya serikali ya sasa ya Cairo imeifanya jamii ya watu wa Misri kupoteza matumaini na kusambaratisha kikamilifu malengo yote ya mapinduzi ya mwezi Januari 2011. Si hayo tu bali inatabiriwa pia kwamba, baada ya kumaliza awamu ya pili ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, Rais Abdel Fattah el-Sisi atafanya mabadiliko ya katiba na kubakia zaidi madarakani katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na hivyo kushuhudiwa tena "Hosni Mubarak mwingine".
Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri anayetajwa kuwa Hosni Mubarak wa pili nchini humo
Katika uwanja huo, Talaat Fahmy, Msemaji wa harakati ya Ikhwanul Muslimin nchini Misri ametahadharisha kwamba serikali ya nchi hiyo inafanya njama za kuwavunja moyo Wamisri. Hata hivyo swali muhimu la kujiuliza ni kwamba, ni kwa nini Rais Abdel Fattah el-Sisi ameamua kufanyike uchaguzi usio na ushindani kiasi hata cha kuwazuia kugombea wanasiasa ambao wana nafasi ndogo sana ya kuibuka na ushindi?
Inaonekana kuwa hatua hizo za el-Sisi zinatokana na mambo mawili ya ndani na nje. Kwa upande wa ndani, jenerali huyo wa zamani hataki kabisa kuona utendaji wake wa miaka minne iliyopita ukijadiliwa na kupewa changamoto na yeyote katika kampeni za uchaguzi. Kuhusiana na suala hilo, Mohammed al-Misri, mwandishi na mhadhiri wa masuala ya vyombo vya habari na utamaduni katika Kituo cha Doha, Qatar ameandika kwamba: "Abdel Fattah el-Sisi anaelewa vyema kwamba, hali ya uchumi na usalama nchini Misri imekuwa mbaya sana ikilinganishwa na wakati alipoingia madarakani. Vilevile mipango ya kiuchumi ya Rais el-Sisi nayo imefeli na ameshindwa kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi. Ughali wa maisha unazidi kuongezeka, kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana kinapanda juu zaidi na umasiki umefika kwenye kiwango cha kutisha nchini humo." Mwisho wa kunukuu.
Muhammad Mursi rais wa zamani wa Misri ambaye anashikiliwa jela.
Ama katika upande wa nje, ukandamizaji wa demokrasia unaofanywa na serikali ya Rais Abdel Fattah el-Sisi unatokana na mienendo ya kindumakuwili ya madola ya Magharibi hususan Marekani kuhusu haki za binadamu na demokrasia. El-Sisi haogopi kwamba, kuitisha uchaguzi wa kimaonyesho na wa kusimamisha mgombea mmoja kutamsababishia mashinikizo ya madola ya Magharibi. Kuhusiana na suala hilo Mohammed al-Misri anasema: "Madikteta waitifaki wa Marekani wanajua kwamba, Washington hufumbia macho demokrasia na haki binadamu kwa ajili ya kuwahami na kuwaunga mkono." Mwisho wa kunukuu.

No comments:

Post a Comment