Monday, January 29, 2018

RAILA ODINGA KUAPISHWA KESHO JUMANNE JAN.30 2018.

   Picha inayohusiana
Kiongozi wa mungano wa upinzani nchini Kenya NASA, Raila Odinga anatarajiwa kuapishwa kama rais wa Jamhuri ya Kenya January 30, 2018 Kuapishwa huko kunatokana na upinzani nchini Kenya kutokukubaliana na ushindi wa rais Uhuru Kenyatta aliyechaguliwa mwishoni mwa mwaka uliopita, ingawa upinzani haukushiriki duru ya pili ya uchaguzi baada ya matokeo ya uchaguzi wa awali kukataliwa na mahakama.
Hata hivyo baadi ya wafuasi wa NASA hawaungi mkono hatua hiyo. Pia wafuasi wa chama tawala cha Jubilee wanapinga vikali kuapishwa kwa Raila Odinga kwa kudai kuwa huenda machafuko yakatokea.
Tukio la kuapishwa kwa Odinga pia linapingwa vikali na Wakenya waishio nje ya nchi hiyo. Kwa upande wa jeshi la polisi nchini Kenya limeimarisha usalama mjini Nairobi katika eneo lililoteuliwa kwa ajili ya tukio hilo la kipekee, na kusisitiza kuwa hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kwenda eneo hilo, ingawa wafuasi wengine wa NASA wanaandaa usafiri wa kuelekea maeneo ya Nairobi kushuhudia sherehe za kuapishwa kwa Odinga.

MAANDAMANO YAENDELEA ETHIOPIA, VIFO VYARIPOTIWA.

Tokeo la picha la ETTIOPIA STRIKES
Wakati mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Afrika AU, ukiendelea mjini Addis Ababa Ethiopia chini ya mwenyekiti wa Umoja huo Paul Kagame, kwa upande mwingine Maandamano yameripotiwa na vyombo vya habari nchini humo ambapo watu kadhaa wameripotiwa kuuwawa katika ghasia hizo zilizofanyika kaskazini mwa nchi hiyo.
Barabara zinaelezwa kuwa ziliwekwa vizuizi huku majengo ya serikali yakielezwa kushambulia. Maandamano hayo yalianza wiki iliyopita baada ya majeshi ya serikali kushambulia waumini wakati wa sherehe za kidini katika mji wa Weldiya, na kusababisha vifo vya watu watano.
Hivi karibuni serikali ya Ethiopia ilitoa uamuzi wa kuwaachia huru maelfu ya wanaharakati, uamuzi ambao haukutuliza maandamanao hayo, ambayo yamekuwa yakifanyika karibu miaka mitatu sasa.

CHINA YAKANUSHA KUFANYA UJASUSI KATIKA MAKAO MAKUU YA AU

China yakanusha kufanya ujasusi katika Makao Makuu ya AU
Balozi wa China katika Umoja wa Afrika AU amekanusha vikali madai ya vyombo vya habari vya Magharibi vilivyodai kuwa nchi hiyo inafanya ujasusi katika Makao Makuu ya AU mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Kuang Weilin amesema kuwa madai ya gazeti la Ufaransa la Le Monde ya kwamba nchi yake inafanya ujasusi katika Makao Makuu ya AU mjini Addis Ababa tangu mwaka 2012 hadi 2017 ni ya kipuuzi na hayana ukweli wowote.
Makao Makuu ya AU mjini Addis Ababa, Ethiopia

Balozi huyo wa China amesema hayo pambizoni mwa kikao cha wakuu wa Umoja wa Afrika kilichofanyika Jumapili na Jumatatu tarehe 28 na 29 Januari 2018 katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Amesema: "Gazeti hilo la Ufaransa limepoteza heshima yake kwa kusambaza madai hayo ya uongo siku ya Ijumaa na kamwe madai kama hayo hayawezi kuharibu uhusiano wa China na Afrika."
Siku ya Ijumaa gazeti la Le Monde la Ufaransa lilinukuu baadhi ya duru za Umoja wa Afrika zikidai kwamba wataalamu wa kompyuta wamegundua kuwa, kwa muda wa mwaka mzima sasa taarifa za watumizi wa kompyuta wa AU zinapelekwa kwa upande wa tatu ulioko mjini Shanghai, China.
Bendera za nchi za Afrika

Kwa upande wake, Umoja wa Afrika umesema unashughulishwa zaidi na uhusiano imara kati ya Afrika na China kuliko madai hayo ya gazeti la Ufaransa.
Itakumbukwa kuwa China ndiye mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa nchi za Afrika.

SAEB ERAKAT: VITENDO VYA MAREKANI VINACHOCHEA MACHAFUKO MASHARIKI YA KATI

Saeb Erakat: Vitendo vya Marekani vinachochea machafuko Mashariki ya Kati
Katibu wa kamati ya utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesema kuwa, hatua na vitendo vya Marekani vimekuwa vikichochea vurugu na machafuko katika eneo la Mashariki ya kati.
Saeb Erakat, amesema bayana kwamba, hatua ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na Beitul-Muqaddas na wakimbizi wa Palestina ni ushahidi wa wazi wa kuchochea na kueneza machafuko na vurugu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Afisa huyo mwandamizi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amebainisha kwamba, uamuzi wa Trump wa kuitambua Beitul Muqaddas kuwa eti ni mji mkuu wa utawala vamizi wa Israel na kutaka uanzishwe mchakato wa kuhamishiwa ubalozi wa Washington katika mji huo unaonyesha msimamo mkali, uenezaji vurugu na machafuko, umwagaji damu na chokochoko alizo nazo rais huyo wa Marekani.
Msikiti wa al-Aqswa, unaopatikana katika mji wa Beitul-Muqaddas Palestina

Saeb Erakat amesema, hatua hiyo ya Trump si chokochoko kwa Palestina tu bali kwa eneo zima la Mashariki ya Kati.
Katibu huyo wa kamati ya utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesisitiza kuwa, njia pekee ya kurejeshwa amani na utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati ni kukomeshwa uvamizi wa Israel na kuimarishwa mamlaka ya kujitawala Palestina mji mkuu wake ukiwa Beitul-Muqaddas.

NJAMA ZA RAIS EL-SISI ZA KUWA MGOMBEA PEKEE WA UCHAGUZI WA RAIS MISRI

Njama za Rais el-Sisi za kuwa mgombea pekee wa uchaguzi wa rais Misri
Nasser Amin, wakili wa Sami Hafez Anan, amesema kuwa, Anan anaendelea kushikiliwa katika jela nchini Misri.
Mkuu wa zamani wa majeshi ya Misri, Sami Hafez Anan hivi karibuni alitangaza azma yake ya kugombea katika uchaguzi ujao wa rais nchini humo lakini amepigwa kalamu na kuzuiwa kushiriki katika zoezi hilo. Anan si mtu wa kwanza kutiwa mbaroni na kuswekwa jela baada ya kutangaza azma yake ya kutaka kugombea kiti cha rais wa Misri. Kabla yake wanasiasa kama Ahmed Shafik, waziri mkuu wa zamani wa Misri na Khalid Ali, wakili na mwanasiasa mashuhuri wa nchi hiyo ama walitiwa jela au waliwekewa mashinikizo makali na kulazimika kutupilia mbali azma yao ya kugombea kiti cha rais wa Misri.
Sami Hafez Anan, aliyewahi kuwa mkuu wa majeshi nchini Misri ametiwa jela baada ya kutangaza azma ya kugombea nafasi ya rais
Katika uwanja huo, serikali ya Cairo ilimzulia kila mmoja wao sababu za kuwaweka jela au kuwekea mashinikizo. Kwa mfano tu mkuu wa zamani wa majeshi Misri yaani Sami Anan, yeye amewekwa jela kwa tuhuma za kukiuka sheria ikiwa ni pamoja na kutopata ridhaa ya jeshi kwa ajili ya kugombea katika uchaguzi wa rais, kughushi nyaraka rasmi na kadhalika kutoa matamshi ya kichochezi dhidi ya jeshi la nchi hiyo. Mienendo hiyo pamoja na mambo mengine, inatajwa na weledi wa mambo kwamba, ni sehemu ya mbinu zinazotumiwa na serikali ya Misri kuhakikisha uchaguzi ujao unafanyika kwa ushiriki wa mgombea mmoja ambaye ni Rais Abdel Fattah el-Sisi pekee, kama ilivyofanyika mwaka 2012 nchini Yemen, wakati Abdrabbuh Mansur Hadi alipokuwa mgombea pekee katika uchaguzi wa rais wa kimaonyesho.
Ahmed Shafik, waziri mkuu wa zamani wa Misri, ambaye naye alikumbwa na misukosuko baada ya kutanganza kugombea kiti cha rais
Ukweli ni kwamba uchaguzi unaopangwa kufanyika tarehe 26 na 28 mwezi Machi mwaka huu nchini Misri, sio uchaguzi huru na halisi, bali ni mchezo wa kutangaza utiifu mpya wa wananchi kwa Rais Abdel Fattah el-Sisi. Mienendo hiyo ya serikali ya sasa ya Cairo imeifanya jamii ya watu wa Misri kupoteza matumaini na kusambaratisha kikamilifu malengo yote ya mapinduzi ya mwezi Januari 2011. Si hayo tu bali inatabiriwa pia kwamba, baada ya kumaliza awamu ya pili ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, Rais Abdel Fattah el-Sisi atafanya mabadiliko ya katiba na kubakia zaidi madarakani katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na hivyo kushuhudiwa tena "Hosni Mubarak mwingine".
Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri anayetajwa kuwa Hosni Mubarak wa pili nchini humo
Katika uwanja huo, Talaat Fahmy, Msemaji wa harakati ya Ikhwanul Muslimin nchini Misri ametahadharisha kwamba serikali ya nchi hiyo inafanya njama za kuwavunja moyo Wamisri. Hata hivyo swali muhimu la kujiuliza ni kwamba, ni kwa nini Rais Abdel Fattah el-Sisi ameamua kufanyike uchaguzi usio na ushindani kiasi hata cha kuwazuia kugombea wanasiasa ambao wana nafasi ndogo sana ya kuibuka na ushindi?
Inaonekana kuwa hatua hizo za el-Sisi zinatokana na mambo mawili ya ndani na nje. Kwa upande wa ndani, jenerali huyo wa zamani hataki kabisa kuona utendaji wake wa miaka minne iliyopita ukijadiliwa na kupewa changamoto na yeyote katika kampeni za uchaguzi. Kuhusiana na suala hilo, Mohammed al-Misri, mwandishi na mhadhiri wa masuala ya vyombo vya habari na utamaduni katika Kituo cha Doha, Qatar ameandika kwamba: "Abdel Fattah el-Sisi anaelewa vyema kwamba, hali ya uchumi na usalama nchini Misri imekuwa mbaya sana ikilinganishwa na wakati alipoingia madarakani. Vilevile mipango ya kiuchumi ya Rais el-Sisi nayo imefeli na ameshindwa kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi. Ughali wa maisha unazidi kuongezeka, kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana kinapanda juu zaidi na umasiki umefika kwenye kiwango cha kutisha nchini humo." Mwisho wa kunukuu.
Muhammad Mursi rais wa zamani wa Misri ambaye anashikiliwa jela.
Ama katika upande wa nje, ukandamizaji wa demokrasia unaofanywa na serikali ya Rais Abdel Fattah el-Sisi unatokana na mienendo ya kindumakuwili ya madola ya Magharibi hususan Marekani kuhusu haki za binadamu na demokrasia. El-Sisi haogopi kwamba, kuitisha uchaguzi wa kimaonyesho na wa kusimamisha mgombea mmoja kutamsababishia mashinikizo ya madola ya Magharibi. Kuhusiana na suala hilo Mohammed al-Misri anasema: "Madikteta waitifaki wa Marekani wanajua kwamba, Washington hufumbia macho demokrasia na haki binadamu kwa ajili ya kuwahami na kuwaunga mkono." Mwisho wa kunukuu.

Sunday, January 28, 2018

BALOZI SOKOINE AKUTANA NA WATANZANIA UBELGIJI

Balozi wa Tanzania nchi Ubelgiji Mh:Edward Joseph Sokoine katikati akiwa na baadhi ya watanzania waliofika jana kwenye kikao cha kusikiliza na kutafutia ufumbuzi kero za watanzania wanaishi mbali na Tanzania. {Picha zote na Maganga One Blog} 
Kiongozi wa Watanzani kitongoji cha Antwerpen nchini Ubelgiji ndugu Joseph Makani akimkaribisha Mh;Balozi na maafisa Ubalozi alioambana nao hapa jana,kutoka kushoto ni Afisa Ubalozi ndugu Shoo na upande wa kulia ni afisa ubalozi ndugu Juma Salum.Kikao kilikwenda vizuri kwani kila mmoja alipewa fursa ya kuuliza maswali. 
Afisa Ubalozi ndugu Juma Salum{kulia}akitoa ufafanuzi wa swali aliloulizwa kuhusu maswala ya hati za kusafiria pindi mtu anapotaka kurudi nyumbani,alielezea kwa kirefu taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili mtu kuepuka usumbufu. 
Mh:Balozi akimsikiliza mmoja wa watanzania ndugu Omari Songambele {hayupo pichani}aliyetaka ufafanuzi kuhusu Uraia Pacha. 
Baadhi ya kina mama wa Kitanzania na nchi jirani walihudhuria mkutano uliowakutanisha na Balozi Sokoine 
Na kwa upande wa kina baba nao walijumuika kwa wingi hapo jana kusikiliza na kutoa maoni kuhusu nchi yao 
Mwenyekiti wa Watanzania nchini Ubelgiji ndugu Mwasha akijitambulisha kwa Mh:Balozi kabla ya kikao hakijaanza rasmi. 
Afisa ubalozi wa Tanzania ndugu Juma Salum,jana alipata nafasi nzuri ya kuyajibu vizuri maswali ya watanzania. Pichani akiendelea kufafanua jinsi ofisi ya balozi inavyofanya kazi zake vyema na kuwasaidia watanzania kwa hali na mali pindi wanapohitaji msaada kwenye ofisi za ubalozi. 
Mmoja wa Watanzania ambaye anaishi nje ya nchi na amefaikiwa kuzaa na mzungu,Pichani wakimsikiliza Mh:Balozi 
Pichani baadhi ya Watanzania wakimsikiliza Mh:Balozi 
Pichani baadhi ya Watanzania wakimsikiliza Mh:Balozi 
Mh:Balozi Sokoine akiwasisitiza Watanzania kuwekeza na kupeleka wawekezaji nyumbani 
Afisa balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji ndugu Shoo akiwaeleza watanzania Fursa za Hisa zitokanazo na mabenki makubwa nchini Tanzania na jinsi ya kujiunga nazo 
Afisa Ubalozi wa Tanzania nduguKabakati nae aliongea na watanzania kuhusu uwekezaji katika sekta mbalimbali,pichani alitoa ufafanuzi wa maswala ya umiliki wa ardhi na mashamba 
Afisa ubalozi na Kanali mstaafu akiwashauri Watanzania kutokusahau walikotoka na kuwasisitiza kuwekeza nyumbani,kutovunja sheria za nchi wanazoishi 
Afisa ubalozi na Kanali mstaafu akiwashauri Watanzania kutokusahau walikotoka na kuwasisitiza kuwekeza nyumbani,kutovunja sheria za nchi wanazoishi 
Watanzania,Wasomali,Warundi , Wacongo na nchi nyingine za jirani kuizunguka Tanzania walihudhuria mkutano wa Balozi wa Tanzania Mh:Balozi Sokoine hapo jana. 
Maganga One Blogger akiwa na maafisa ubalozi wa Tanzania wakibadilishana mawazo 
Maganga One Blogger alipata fursa ya kuongea na Mh:Balozi na kumueleza changamoto za Watanzania ughaibuni,Mh:Balozi Sokoine aliahidi kuwasaidia Watanzania kadri atakavyoweza na kutatua kero zao. 
Mh:Balozi Sokoine akiagana na Omary Songambele mara baada ya kikao kumalizika hapa jana.pembeni mwa balozi ni Dulla Criss Cross mmoja wa viongozi wa Antwerpen 
Shabiki namba moja wa Simba ughaibuni ndugu Nyambi kushoto akiwa na dada wa Kitanzania wakipata picha ya kumbukumbu 
Kutoka kushoto ni Afisa Balozi na kanali mstaafu,ndugu Omary Songambele,Mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa Kassim Manara,Afisa ubalozi ndugu Kabakati na Mh:Balozi Edward Sokoine hapo jana jijini Antwerpen katika kikao cha kuzungumzia maendeleo ya nchi ya Tanzania.

MPINZANI WA EL SISI KATIKA UCHAGUZI UJAO MISRI ATUPWA KATIKA JELA YA KIJESHI

Mpinzani wa el Sisi katika uchaguzi ujao wa Misri atupwa katika jela ya kijeshi
Wakili wa mkuu wa zamani wa jeshi la Misri ambaye ametangaza kuchuana na Rais Abdul Fattah el Sisi katika uchaguzi ujao wa rais nchini humo amesema kuwa, mteja wake emepelekwa katika jela ya kijeshi.
Habari hiyo imetangazwa leo na gazeti la Ra'y al Yaum na kumnukuu Naser Amin, wakili wa Sami Hafez Anan, mkuu wa zamani wa jeshi la Misri akiandika katika ukurasa wake wa Facebook wamba ameruhusiwa kwenda kuonana na Anan katika jela ya kijeshi.
Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri

Komandi Kuu ya vikosi vya ulinzi vya Misri, Jumanne ilivyopita ilitoa tamko na kumlaumu Anan kwa kutangaza kushiriki katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo. Aidha komandi hiyo ilimtuhumu Anan kuwa amevunja sheria na kutoa maneno ya kichochezi dhidi ya vikosi vya ulinzi vya Misri.
Tuhuma nyingine alizobebeshwa Sami Hafez Anan baada ya kutangaza kuwa atachuana na Rais Abdul Fattah el Sisi katika uchaguzi ujao ni pamoja na madai ya kughushi nyara na vyeti rasmi.
Tayari Ahmad Shafiq, waziri mkuu wa zamani wa Misri ametangaza kujitoa katika kinyang'anyiro hicho.
Khaled Ali, mwanasiasa mwingine aliyetangaza kuchuana na el Sisi naye ameshatangaza kujitoa katika kinyang'anyiro hicho. Kwa hali hiyo, hivi sasa Rais wa Misri Abdul Fattah el Sisi amebakia peke yake katika uchaguzi huo bila ya mpinzani yeyote.
Uchaguzi wa Rais wa Misri unatarajiwa kufanyika kati ya tarehe 26 na 28 Machi mwaka huu wa 2018

MKUTANO WA WAKUU WA AFRIKA UNAENDELEA MJINI ADDIS ABABA, ETHIOPIA

Mkutano wa wakuu wa Afrika unaendelea mjini Addis Ababa, Ethiopia
Mkutano wa 32 cha Umoja wa Afrika (AU) umeanza huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia kwa kuhudhuriwa na viongozi wengi wa nchi za Kiafrika.
Vikao vya duru ya 32 ya Mkutano wa Umoja wa Afrika vimeanza leo Jumapili kwa kuhudhuriwa na viongozi wengi wa nchi za Afrika. Vikao hivyo vimeendeshwa katika hali ya faragha na duru ya 32 ya Mkutano wa Viongozi wa Afrika imepangwa kufunguliwa baada ya kumalizika vikao hivyo.   
Duru ya 32 ya Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Afrika waanza Addis Ababa
 
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye anahudhuria katika mkutano huo amesisitiza kuwa ipo haja ya kuungwa mkono nchi za bara la Afrika ili kuweza kuwa na amani na kustawisha taasisi za nchi hizo. Guterres amesema kuwa, askari jeshi wa Umoja wa Mataifa wataendelea na shughuli zao barani Afrika. 
Duru ya 32 ya Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Afrika itadumu kwa siku mbili; ambapo washiriki katika mkutano huo watajadili na kuchunguza  mizozo na changamoto kuu zinazozikabili baadhi ya nchi za Afrika, ugaidi, na suala la kuimarisha mashirikiano kati ya nchi hizo chini ya kaulimbiu "Ushindi katika mapambano dhidi ya ufisadi na mageuzi Afrika."

POLISI UJERUMANI YAWATAWANYA WAANDAMANAJI TAKRIBANI 15,OOO

Deutschland | Polizei löst Kurden-Demo in Köln
Chanzo, DW.
Jeshi la Polisi nchini Ujerumani limewatawanya  waandamanaji takribani 15,000 wa kikurdi waliokuwa wamebeba mabango yanayoonesha  nembo  za  chama  cha  wafanyakazi wa  Kikurdi PKK, zilizopigwa marufuku  nchini  humo.
Katika taarifa zilizoripotiwa na shirika la habari la Ujerumani DW, zilieleza kuwa Maandamano  hayo yaliyofanyika mjini Kolon-Ujerumani, yalitayarishwa  na  chama cha wafanyakazi cha NAV-DEM cha Wakurdi  ambacho  kinaelezwa  kuwa na ukaribu na chama kilichopigwa  marufuku  cha  PKK. Chama hicho kinaelezwa pia kupigwa  marufuku nchini Uturuki pamoja na washirika wake wa mataifa  ya magharibi  kwamba ni kundi la kigaidi. Watu  wawili walikamatwa  katika  maandamano  hayo, ambayo yaliyokuja wiki moja baada ya vikosi maalum vya jeshi la Uturuki na waasi ambao ni washirika wa Uturuki nchini Syria, kufanya mashambulizi yakuwalenga wanamgambo wa Kikurdi wa kundi la vikosi vya ulinzi wa umma YPG, kaskazini mwa Syria.
Hakuna  tukio  lililoripotiwa  mara  moja, japo hali iliripotiwa kuendelea kuwa tete, kwa mujibu wa msemaji wa polisi ambaye aliongeza kwamba kulikuwa na wasi wasi juu  yakuzuka mapambano kati ya waandamanaji  na polisi.

Thursday, January 25, 2018

TRUMP AWASILI DAVOS

Akishikilia silaha yake ya nadharia ya "Amerika kwanza" rais Donald Trump aliwasili Uswisi kutetea ajenda yake hiyo ya kiuchumi katika  kongamano la kiuchumi ambalo linasisitiza biashara na ushirikiano wa kimataifa.
Schweiz Ankunft Trump in Zürich (Getty Images/AFP/N. Kamm)
Trump  aliwasili  mjini  Zurich kabla  ya  muda  uliopangwa  na  mara moja  alipanda  katika  helikopta  ya  Marekani  kwa  ajili  ya  safari kwenda  Davos, ambako  kongamano la  kiuchumi  duniani linafanyika. Safari  hiyo  ya  takriban dakika  40 ilimchukua  Trump akipita  katika  mandhari  ya  nchi  iliyofunikwa  na  barafu , hapa  na pale  kukiwa  na  nyumba , milima  iliyovunikwa  na  theluji  pamoja na  ziwa zililoganda  barafu.
Schweiz, World Economic Forum in Davos (picture-alliance/D.Keyton) Eneo la Davos lililofunikwa na barafu
Wakati  Trump  aliposhuka  kutoka  katika  helikopta  hiyo  mjini Davos, aliwaangalia  wasaidizi  wake  ambao  walimshika  mkono wakati  akitembea  katika  eneo  la  kutua  na  ambalo  limejaa theluji hadi  katika  gari  yake iliyokuwa  ikimsubiri.
Wakati  rais  Trump  anatarajiwa  kutangaza  kwamba  Marekani  iko wazi  kwa  ajili  ya   kufanya biashara , kuhudhuria  kwa  rais  huyo ambaye  anaelemea  kulinda  masoko  ya  nchi  yake  katika mkusabyiko  huko  wa  kila  mwaka  kwa  watu  mashuhuri , wanasiasa  na  wafanyabiashara  ambao  hupendelea  biashara huria , amewashitua  wengi.
Uamuzi  wake  wiki  hii  kutia  saini matumizi  ya kodi  mpya  inayoimarisha  viwanda  vya  Marekani imezusha  wasi  wasi  mpya  juu  ya  mwelekeo  wake  wa  siasa  za kizalendo  zaidi.
USA Donald Trump (picture-alliance/AP Photo/C. Kaster) Rais wa Marekani Donald Trump
Trump atamba
"Ninakwenda  Davos  hivi  sasa  kuwezesha  watu  kuwekeza  nchini Marekani," Trump  alisema  jana  kabla  ya  kupanda  ndege  kwenda barani  Ulaya. "Nitawaambia : njoni  Marekani. Mna  fedha  nyingi." Lakini  sifikiri  kama  ni  muhimu  kwenda, kwasababu  wanakuja, wanakuja kwa  haraka  sana."
Katika  maelezo  yake  katika  ukurasa  wa  Twitter aliyoandika kabla  kuondoka  Ikulu  ya  Marekani  ya  White House Trump alisema, "Uchumi  wetu unakua  kwa  kasi na  kwa  kila  kitu ninachofanya , utaendelea  vizuri  tu.. nchi  yetu  hatimaye inashinda tena!"
Waziri  mkuu  wa  Uingereza  Theresa  May  alipoulizwa  kuhusu iwapo  atazungumza  na  Trump  kuhusu biashara  huru , alisema.
"Biashara  huru  ni  mada  ambayo  niliijadili  na  rais hapo  zamani. Tuna  shauku  kubwa  kwamba  tutaweza kufanya  hivyo na Marekani wakati  tutakapoondoka  katika  Umoja  wa  Ulaya. Wanashauku  kubwa  kwa  hilo, na sisi  pia tunashauku na  tayari tunalifanyia  kazi juu  ya  vipi tutatekeleza  hilo".
Theresa May beim Weltwirtschaftsforum in Davos (Reuters/D. Balibouse) Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May
Waziri  wa  fedha  wa  Marekani  Steven  Mnuchin  aliwasili  mjini Davos  kabla  ya  Trump  na  kusisitiza  kwamba  Marekani  inaunga mkono  biashara  huru.
Waziri  wa  biashara  wa  Marekani  Wilbur Ross amedai  kuwa kodi mpya  nchini  Marekani  kwa  vifaa  vinavyoagizwa  kutoka  nje  vya nishati  ya  jua , solar pamoja  na  mashine  kubwa  za  kufulia zina lenga  kupambana  na  tabia  ambazo  hazistahili za   baadhi  ya mataifa  na  sio kulinda  masoko. Pamoja  na  hayo  Ross  alikiri kwamba  China  inaweza  kujibu  hali  hiyo  kwa  kuweka kodi  zake kwa  biadhaa  za  Marekani.

Wednesday, January 24, 2018

BARAZA LA USALAMA LINAKUTANA LEO KUJADILI KADHIA YA PALESTINA

  • Baraza la Usalama linakutana leo kujadili kadhia ya Palestina
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana leo Alkhamisi katika kikao chake cha dharura kwa shabaha ya kujadili kadhia ya Palestina.
Tayseer Jaradat, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Palestina amesema kuwa, kikao hicho cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kinafanyika kwa ombi la Palestina.
Riyadh Mansour, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, lengo la kikao hicho ni kulikumbusha majukumu yake Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na Palestina.
Itakumbukwa kuwa, Disemba 21 mwaka jana, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha kwa wingi wa kura azimio la kuiunga mkono Beitul-Muqaddas.
Beitul-Muqaddas, Palestina
Kwa mujibu wa azimio hilo, Umoja wa Mataifa ulitangaza kwamba, hauitaimbua Beitu-Muddas kama mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel.
Tarehe 6 mwezi uliopita wa Disemba, Rais Donald Trump wa Marekani aliitangaza Quds Tukufu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel na akatoa amri ya kufanyika taratibu za kuuhamishia mjini humo ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv, mji mkuu wa utawala dhalimu wa Kizayuni.
Hii ni katika hali ambayo, mji wa Quds kunakopatikana Masjid Aqswa, kibla cha kwanza cha Waislamu ni sehemu isiyotenganishika na Palestina na ni miongoni mwa maeneo matatu muhimu na matakatifu baada ya Makka na Madina.

RUSSIA NA SYRIA ZAKANUSHA MADAI YA MAREKANI KUHUSU SILAHA ZA KEMIKALI

Russia na Syria zakanusha madai ya Marekani kuhusu silaha za kemikali
Russia na Syria zimekadhibisha madai yaliyotolewa na Marekani na Ufaransa kwamba serikali ya Damascus imetumia silaha za kemikali katika mashambulizi yake, zikisisitiza kuwa tuhuma hizo zinapania kutia vizingiti katika juhudi za kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya amani mgogoro unaoshuhudiwa katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Taarifa ya serikali iliyopeperushwa na shirika rasmi la habari la Syria SANA imesema madai hayo ya US na Ufaransa ni urongo wa wazi ambao hauna lengo jingine ghairi ya kuvuruga mkondo wa kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa miaka kadhaa wa Syria.
Imeongeza kuwa, Syria ilikabidhi mrundiko wa silaha zake zote za kemikali mwaka 2014, kwa Umoja wa Mataifa na Shirika la Kupambana na Silaha za Kemikali OPCW, ambapo zote ziliharibiwa.
Makao Makuu ya Shirika la Kupambana na Silaha za Kemikali OPCW
Wakati huo huo, Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema katika mahojiano na shirika la habari la Interfax kwamba, Marekani inaeneza propaganada na ripoti ambazo hazijathibitishwa, ili kutia viunzi katika jitihada za Moscow za kutatuliwa mzozo wa Syria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson na mwenzake wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian siku ya Jumanne wakiwa mjini Paris walidai kuwa, Moscow inabeba dhima ya eti kutumiwa silaha za kemikali nchini Syria na eti kwamba wahusika wanapaswa kuwajibishwa na kuwekewa vikwazo.

PAPA ATOA WITO WA KUPIGWA VITA UBAKAJI NA KUNAJISIWA WATOTO

Papa atoa wito wa kupigwa vita ubakaji na kunajisiwa watoto
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani amesisitiza juu ya ulazima wa kuchukuliwa hatua za dhati za kukabiliana na vitendo vya ubakaji na kunajisiwa watoto.
Papa Francis amesema hayo baada ya kurejea kutoka katika safari yake ya Amerika ya Latini ambayo iligubikwa na kashfa za ngono katika makanisa ya katoliki.
Sambamba na kutahadharisha kuhusiana na vitendo vya kubakwa na kunajisiwa watoto wadogo amesisitiza kwamba,  wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua.
Itakumbukwa kuwa, akiwa katika safari yake nchini Chile, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani alieleza masikitiko yake kutokana na kashfa za ngono na ulawiti zinazolikabili kanisa hilo nchini humo.
Papa Francis akiwasili Bangladesh
Katika hotuba yake ya kwanza akiwa pamoja na Rais Michelle Bachelet wa Chile, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani alisema kuwa, kashfa hizo za ngono zimelipaka matope kanisa hilo.
Kashfa mbalimbali za kimaadili na kifedha zilizoikumba Vatican na Kanisa Katoliki katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikigonga vichwa vya habari na kuwa gumzo kubwa lisilokwisha duniani. 
Kuna mamia ya kesi za ubakaji na ulawiti zinazowakabili makasisi wa kanisa hilo, ambazo zimerundikana katika mahakama za Ulaya na Marekani zikisubiri kufanyiwa uchunguzi, jambo ambalo limeshusha hadhi ya Kanisa Katoliki Duniani.