Sunday, December 31, 2017

KOREA KASKAZINI YAAPA KUIMARISHA ZANA ZAKE ZA NYUKLIA MWAKA 2018

Korea Kaskazini yaapa kuimarisha zana zake za nyuklia mwaka 2018
Korea Kaskazini imeapa kufanyia majaribio zaidi ya zana zake za nyuklia mwaka 2018 huku ikisisitiza kuwa uwezo wake hauwezi kuangamizwa au kuvurugwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kupitia shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA, wakuu wa Korea Kaskazini wameilamu Marekani kwa kuendeleza njama dhidi yake katika sekta za kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kidiplomasia katika mwaka huu unaomalizika wa 2017. Taarifa hiyo imesema pamoja na kuwepo njama hizo za Marekani Korea Kaskazini haikusita katika mkondo wake na ina yakini ya kupata ushindi.
Aidha Korea Kaskazini imesema itazidi kuimarisha uwezo wake wa kujihami ili kukabiliana na vitisho vya nyuklia vya Marekani. Wakuu wa Pyongyang pia wameilaumu vikali Marekani kwa kuendeleza uchochezi kupitia vitisho vya nyuklia na mazoezi ya kijeshi katika mipaka yake.
Rais Donald Trump wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini  Kim Jong-u
Septemba mwaka huu, Korea Kaskazini ilifanyia majaribio kwa mafanikio bomu la nyuklia, hilo likiwa ni jaribio la sita la aina hii kufanywa na nchi hiyo.
Marekani, ambayo ni mchochezi mkuu wa mivutano kwenye eneo la Peninsula ya Korea imekuwa kila mara ikishikilia Korea Kaskazini isimamishe majaribio yake ya nyuklia, lakini viongozi wa Pyongyang wanasisitiza kwamba madamu Marekani na waitifaki wake wanaendelea kutoa vitisho dhidi ya Korea Kaskazini, nchi hiyo nayo itaendelea kujiimarisha kijeshi.

No comments:

Post a Comment