Tuesday, December 12, 2017

ZAIDI YA WATOTO LAKI NNE DRC WANAKABILIWA NA HATARI YA KIFO KUTOKANA NA UTAPIAMLO

Zaidi ya watoto laki nne DRC wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na utapiamlo
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF limeonya kuwa, zaidi ya watoto laki nne walio chini ya umri wa miaka mitano wanakumbwa na utapiamlo mkubwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imetahadharisha kuwa,  watoto hao wanaweza kufariki dunia katika kipindi cha miezi michache kutoka sasa kama hatua za haraka hazitachukuliwa.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF limetangaza katikka taarifa yake kwamba, mgogoro uliopo kwenye jimbo la Kasai na kudorora kwa shughuli za kilimo ni sababu kubwa ya tatizo hilo. 
Aidha shirika hilo la kimataifa limesema kuwa, licha ya usalama kuboreka katika baadhi ya maeneo na hata raia kuanza kurejea katika makazi yao, lakini hali ya kibinadamu bado ni mbaya  kutokana na kukosekana huduma muhimu.
Nembo ya UNICEF
Ripoti ya UNICEF inaonyesha kuwa, baadhi yya maeneo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hayana kabisa huduma za afya kutokana na baadhi ya vituo kuporwa vifaa vyake au kuharibiwa.
Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa uwanja wa mapigano na mauaji kwa miaka 20 sasa. Kushindwa jeshi la serikali na askari wa kofia buluu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa kukabiliana vilivyo na waasi ni moja ya sababu kuu za kukosekana utulivu na amani katika maeneo hayo kwa miaka 20 sasa.

No comments:

Post a Comment