Jumuiya ya Kiislamu ya al Wifaq ya Bahrain
imelaani hukumu iliyotolewa na mahakama ya kijeshi ya nchi hiyo kwa raia
wa nchi hiyo na kuitaja kuwa ni batili.
Jumuiya hiyo imesisitiza leo
ikijibu hatua ya mahakama kuu ya kijeshi ya Bahrain ya kuwakatia hukumu
ya kifo raia wa nchi hiyo kwamba kutishiwa kuuawa, kulazimishwa kukiri
chini ya mateso kama kuadhibiwa kwa kushtushwa na umeme, kutishia
kuwabaka ndugu na familia, kutekwa na kutiwa mbaroni kwa kificho kuwa ni
vitendo visivyo vya kibinadamu wanavyofanyiwa raia wa Bahrain.
Taaarifa ya Jumuiya ya Kiislamu ya al Wifaq imeongeza kuwa jamii ya
kimataifa inapasa kuvunja kimya chake na kujiondoa katika kifungo cha
wenzo wa mashinikizo wa mafuta na dola, na badala yake ionyeshe msimamo
na ichukue hatua mkabala na maafa na jinai hizo zinazojiri huko Bahrain
chini ya kivuli cha kukosekana uadilifu.
Jumuiya ya al Wifaq imesisitiza kuwa
fikra za ulipizaji kisasi haziwezi kudhibiti irada ya wananchi na kwamba
vyombo vya mahakama vinawanyima wananchi wa Bahrain haki zao za msingi
huku mahakama za kijeshi na vyombo vya usalama vikigeuzwa na kutumiwa
kama wenzo na utawala ulioko madarakani katika kuwatesa raia wanaopinga
utawala wa kidikteta na wa kifisadi wa nchi hiyo. Mahakama ya kijeshi ya
Bahrain leo Jumatatu imewahukumu kunyongwa raia sita wengine wa nchi
hiyo kwa tuhuma zisizo na msingi kwamba walihusika katika kupanga njama
ya kumuuwa Sheikh Khalifa bin Ahmed Al Khalifah kamanda mkuu wa jeshi la
nchi hiyo na vitendo vingine vya kigaidi.
No comments:
Post a Comment