Saudi Arabia ilimdhalilisha vibaya sana
Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri katika safari yake ya hivi karibuni
mjini Riyadh wakati alipolazimishwa kusoma taarifa ya kujiuzulu mbele ya
televisheni.
Gazeti
la The New York Times limeandika Hariri alikuwa ni kama mateka na
alilazimishwa kusoma barua ya kujiuzulu akiwa sehemu isiyojulikana
Saudia mnamo Novemba 4 ambapo pia alitoa tuhuma zisizo na msingi kuwa
eti Iran na Hizbullah zinaingilia masuala ya ndani ya eneo na hivyo
amelazimika kujiuzulu.
Lakini
Rais wa Lebanon Michel Aoun alishuku kuwa Hariri alijiuzulu chini ya
mashinikizo na hivyo hakukubali hatua hiyo na alimtaka arejee nyumbani
kutoka Saudia. Vyombo vya usalama vya Lebanon vilithibitisha kuwa Hariri
alilazimishwa kujiuzulu na hatimaye alirejea Lebanon Novemba 22 baada
ya upatanishi wa Ufaransa. Hariri hatimaye alibatilisha uamuzi wake wa
kujiuzulu Disemba 5.
Taarifa zinasema kuwa Hariri
alipowasili Saudia alidhani atapokewa rasmi lakini alipofika katika
kasri ya mfalme alipokonywa simu zake za mkononi na walinzi wake
walitimuliwa huku wakitukanwa na maafisa wa usalama wa Saudia. Hapo
alikabidhiwa barua ya kujiuzulu na akaambiwa aisome katika televisheni
ya taifa ya Saudia. Badala ya kuenda hotelini alipelekwa katika nyumba
maalumu iliyokuwa chini ya ulinzi mkali wa askari wa Saudia na wala
hakuruhusiwa kuonana na mke na watoto wake. Lengo la Saudia lilikuwa ni
kupunguza ushawishi wa harakati ya Hizbullah katika serikali ya Lebanon
lakini njama hizo zimegonga mwamba.
No comments:
Post a Comment