Kundi la kigaidi la ISIS limedai kuhusika na
hujuma ya kigaidi iliyolenga Idara ya Usalama wa Taifa ya Afghanistan
katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul.
Watu
wasiopungua sita wameuawa katika hujuma hiyo huku wengine wawili
wakijeruhiwa baada ya gaidi aliyekuwa amejishehenesha mabomu kujiripua
katika mlango mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (NDS) mjini Kabul.
Hujuma
hiyo imetokea wakati wafanyakazi walipokuwa wakiwasili katika ofisi kwa
ajili ya kuanza kazi. Taarifa zinasema mwanamke mmoja ni miongoni mwa
waliouawa katika hujuma hiyo.
Wiki
iliyopita kituo kimoja cha Idara ya Usalama wa Taifa cha Afghanistan
kilishambuliwa na magaidi na katika makabiliano hayo magaidi watatu
waliuawa baada ya masaa matatu ya mapigano.
Hayo yanajiri wakati Mjumbe maalumu wa
rais wa Russia nchini Afghanistan akiwa ametoa indhari kuwa wanachama
zaidi ya elfu kumi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la ISIS hivi sasa
wako nchini Afghanistan na kwamba idadi yao inazidi kuongezeka kutokana
na kubadilisha maskani yake kundi hilo baada ya kusambaratishwa katika
nchi za Syria na Iraq.
Zamir
Kabulov ametoa indhari hiyo katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la
habari la Sputnik na kuongeza kuwa Russia ina wasiwasi wa kupanuka
harakati za ISIS kwenye mikoa ya kaskazini mwa Afghanistan inayopakana
na Tajikistan na Turkmenistan.
Ikumbukwe
kuwa hivi sasa kuna wanajeshi wapatao 11,000 wa Marekani nchini
Afghanistan. Washington na washirika wake katika muungano wa kijeshi wa
NATO waliivamia kijeshi nchi hiyo mwaka 2001 kwa kisingizio cha
kupambana na ugaidi lakini si tu kuwa hawajafanikiwa bali pia ugaidi
umeongezeka nchini humo.
No comments:
Post a Comment