Jeshi la Uganda limetangaza habari ya kuua
wanachama wasiopungua 100 wa kundi la waasi wa ADF katika makabiliano
makali yaliyojiri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na Jeshi la Ulinzi la Uganda
UPDF imesema kuwa, vikosi vyake vimefanya mashambulizi ya angani na
ardhini dhidi ya maficho ya waasi hao katika mpaka wa nchi hiyo ya
Afrika Mashariki na Kongo DR, na kufanikiwa kuua zaidi ya 100 miongoni
mwao na kujeruhi wengine wengi.
Hujuma hii dhidi ya waasi wa ADF imefanyika siku chache baada
ya Uganda na Kongo DR kukubaliana kuimarisha utaratibu wa mawasiliano na
kupeana taarifa za kiintelijensia kwa ajili ya kupambana na waasi hao
wanaotokea Uganda, ambao wanaendesha harakati zao mashariki mwa DRC.
Itakumbukwa kuwa, askari 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
waliuawa mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba, na 44 wengine walijeruhiwa
katika kambi ya Semuliki mkoani Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia hujuma ya waasi hao wa ADF.
Wanajeshi waliouawa walikuwa ni sehemu ya askari 3,000 wa timu ya
kulinda amani ya Umoja wa Mataifa MONUSCO yenye askari kutoka Tanzania,
Malawi na Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment