Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu
ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameashiria kufanyika Kikao cha Baraza la
Usalama la umoja huo kuhusu azimio nambari 2231 la mapatano ya nyuklia
ya Iran na kusema washiriki wa kikao hicho walitangaza kuunga mkono
mapatano hayo na kwamba kikao hicho kilithibitisha namna Marekani
ilivyotengwa.
Siku ya Jumanne, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
liliitisha kikao kujadili mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana
kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA yaliyofikiwa mwaka
2015 baina ya Iran na Russia, China, Uingereza, Ufaransa, Marekani na
Ujerumani. Baada ya mapatano hayo, Baraza la Usalama lilipasisha azimio
nambari 2231 kuhusu kuunga mkono utekelezwaji mapatano hayo.
Katika kikao cha Jumanne, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa
Nikki Haley alitengwa na washiriki wote wa kikao wakiwemo Jeffrey
Feltman Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Joanne Adamson
Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya ambao wote waliunga mkono JCPOA.
Akizungumza katika kikao hicho, Gholamali Khoshroo mwakilishi wa
kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa, Iran, kinyume
na Marekani, inafungamana kikamilifu na JCPOA na hilo limethibitishwa
katika ripoti 9 za Wakala wa Nyuklia wa Umoja wa Mataifa IAEA.
Mwakilishi wa Iran pia akijibu madai ya Nikki Haley katika kikao
hicho kuwa eti Iran inatoa msaada wa kijeshi kwa Yemen alisema:
"Mwakilishi wa Marekani anatoa tuhuma bandia dhidi ya Iran pasina
kuashiria namna harakati za kijeshi za serikali yake zinavyovuruga
uthabiti wa eneo kwa kuuza silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola na
kukabidhi baadhi ya silaha hizo kwa makundi ya kigaidi kama vile ISIS au
Daesh."
Katika kikao hicho Feltman pia amepinga madai hayo ya Haley.
Ikumbukwe kuwa tokea Machi 2015 hadi sasa, Marekani imekuwa ikiunga
mkono hujuma ya kinyama ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen na imekuwa ikiupa
utawala huo wa Riyadh silaha ambazo hadi sasa zimewaua Wayemen zaidi ya
13,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.
No comments:
Post a Comment