Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya
Iran leo wamepitisha mpango wa dharura wa kuunga mkono Mapinduzi ya
Kiislamu ya watu wa Palestina na kusisitiza kwamba Baitul Muqaddas
utakuwa mji mkuu wa kudumu wa nchi ya Palestina.
Mpango huo wa dharura umepitishwa kwa kura 187 za ndiyo, 15 za
hapana huku wabunge tisa kati ya wabunge wote 233 waliohudhuria kikao
hicho cha wazi cha bunge la Iran wakiamua kutopiga kura.
Mpango huo uliopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
unaunganishwa kwenye Ibara nambari moja ya sheria ya kuunga mkono
Mapinduzi ya Kiislamu ya watu wa Palestina.
Mpango huo utawasilishwa kwenye kamati husika ya Majlisi ya Ushauri
ya Kiislamu na kuwekwa kwenye ajenda za kujadiliwa na kupitishwa rasmi
na bunge hilo ndani ya muda wa masaa 48 yajayo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muungaji mkono thabiti wa mapambano ya
Wapalestina na imekuwa ikitoa wito kwa Waislamu wote duniani kuungana
dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel ambao Tehran haiutambui
asilani kuwa ni moja ya nchi za ulimwengu.
Itakumbukwa kuwa tarehe 6 Desemba, Rais Donald Trump wa Marekani
aliamsha hasira za walimwengu kwa kutangaza kuitambua Baitul Muqaddas
kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel na kuagiza zichukuliwe hatua
za maandalizi ya kuuhamishia katika mji huo ubalozi wa Marekani ulioko
Tel Aviv.
Hata hivyo siku ya Alkhamisi iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa lilipitisha azimio kwa wingi mkubwa wa kura 128 za 'ndiyo' dhidi
ya 9 tu za 'la' kupinga tangazo hilo la rais wa Marekani na kumtaka
abadilishe uamuzi wake huo.
Kwa mujibu wa azimio hilo, Umoja wa Mataifa hautoitambua Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.../
No comments:
Post a Comment