Saturday, December 16, 2017

UINGEREZA YALAUMIWA KWA KUZIUZIA SILAHA TAWALA KANDAMIZI KAMA SAUDIA

Uingereza yalaumiwa kwa kuziuzia silaha tawala kandamizi kama Saudia
Mjumbe wa ngazi ya juu wa harakati ya kupambana na biashara ya silaha nchini Uingereza amesema London inaiunga mkono na kuihami Saudi Arabia na tawala nyingine kandamizaji duniani.
Andrew Smith ameliambia Shirika la Habari la Iran (IRNA) kwamba, asilimia 60 ya silaha za Uingereza zinauzwa kwa tawala zinazokiuka haki za binadamu na kwa watawala madikteta wa Mashariki ya Kati.
Smith ameongeza kuwa, serikali kama ya Uingereza ambazo zimekuwa zikimimina silaha katika maeneo yenye vita zinaiangalia maudhui hiyo kwa mtazamo wa kibiashara ili ziweze kujikurubisha zaidi kwa tawala kama Saudi Arabia na Bahrain.
Ameongeza kuwa Uingereza inaendelea kuiuzia silaha Saudi Arabia licha ya mauaji na mgogoro mkubwa wa kibinadamu unaoshuhudiwa sasa nchini Yemen ambao umesababishwa na mashambulizi na mzingiro wa serikali ya Riyadh dhidi ya nchi hiyo. 
Andrew Smith ameongeza kuwa, tangu mwanzoni mwa mgogoro wa Yemen, Uingereza imeuizia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya pauni bilioni 4 na milioni mia 600. 
Vilevile harakati inayopinga biashara ya silaha nchini Uingereza imewasilisha mashtaka dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Theresa May na kutoa wito wa kusitishwa mara moja mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia.

No comments:

Post a Comment