Mkuu wa Majeshi ya utawala haramu wa Kizayuni
wa Israel amesema kuwa, ni kwa maslahi ya utawala huo ikiwa utaendelea
kujitenga mbali na vita vyovyote na Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya
nchini Lebanon.
Gadi Eizenkot, aliyasema hayo jana
Alkhamisi katika mahojiano na mtandao wa habari wa Kizayuni wa Walla na
gazeti la utawala huo la Yedioth Ahronoth na kuongeza kuwa, harakati ya
Hizbullah ndio adui mkubwa na hatari anayeitia wasi wasi mkubwa Israel,
hasa kwa kuzingatia kuwa ina uwezo mkubwa wa kijeshi huku ikiwa na
ngome kadhaa za kijeshi Lebanon na Syria kiasi cha kuifanya iwe jeshi
kubwa.
Amesisitiza kuwa, harakati hiyo ya
muqawama imekuwa ikipambana nchini Syria kwa miaka kadhaa sasa huku
ikiwa na vikosi kamili vya kivita sambamba na kutoa misaada ya kijeshi
na intelejensia za kivita kwa jeshi la Syria. Ameongeza kuwa, hata kama
jeshi la Israel lina nguvu, lakini linatakiwa liendelee kujizuia
kuanzisha vita vyovyote na harakati hiyo ya Kiislamu. Mkuu wa Majeshi ya
utawala haramu wa Kizayuni wa Israel sambamba na kujaribu kuwapa
utulivu Wazayuni kwamba hivi sasa eti ardhi za Palestina zinazokaliwa
kwa mabavu ( Israel) kuna usalama na kwamba, jeshi la Israel limejiandaa
kukabiliana na aina yoyote ya changamoto na tishio dhidi yake, amesema
kuwa, ni lazima utengamano uliopo kwa sasa uendelee kuwepo badala ya
kuingia vitani na Hizbullah.
Itakumbukwa kuwa katika vita vya siku 33
vya mwaka 2006 kati ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na harakati
ya muqawama ya Hizbullah, Israel ilipata hasara kubwa na kulazimika
kurudi nyuma. Katika sehemu nyingine Gadi Eizenkot amesema kuwa uwepo wa
serikali ya mamlaka ya ndani ya Palestina inaoongozwa na Mahmoud Abbas
ni kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni kwa kuwa kuna mahusiano mazuri ya
kiusalama kati ya Israel na serikali hiyo.
No comments:
Post a Comment