Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, utatuzi wa suala la ugaidi unahitajia ushirikiano wa kimataifa.
Dakta Ali Larijani alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwa pamoja na Siegfried Bracke, Spika wa Bunge la Ubelgiji ambapo alisisitiza juu ya kuweko ushirikiano kati ya Tehran na Brussels katika nyanja mbalimbali hususan katika migogoro ya Mashariki ya Kati ikiwemo ya Yemen na Myanmar.
Spika Larijani amesema kuwa, ana matumaini Mabunge ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ubelgiji yatapanua zaidi wigo wa mazungumzo na ushirikiano hususan katika masuala ya haki za binadamu. Aidha amesema kwamba, ana matarajio safari ya Spika wa Bunge la Ubelgiji hapa Tehran itafungua zaidi milango ya ushirikiano wa kiuchumi na masuala mengine.
Kwa upande wake Siegfried Bracke Spika wa Bunge la Ubelgiji sambamba na kuashiria kwamba, nchi yake haikubaliani na siasa zote za Marekani amesisitiza kwamba, ofisi ya Umoja wa Ulaya inapaswa kufunguliwa haraka iwezekanavyo mjini Tehran.
Spika wa Bunge la Ubelgiji sambamba na kukaribisha kwa mikono miwili ustawishaji ushirikiano na Iran amesisitiza juu ya kuondolewa vizingiti vilivyoko katika uwanja huo.
Kadhalika Siegfried Bracke sanjari na kuashiria kwamba, viongozi wa Iran na Ubelgiji wanaona kuna umuhimu wa kustawishwa zaidi ushirikiano wa pande mbili katika vita dhidi ya ugaidi amesema kuwa, polisi wa pande mbili wamekuwa na mazungumzo ya ngazi za juu kabisa.
No comments:
Post a Comment