Sambamba na kutangazwa majina mapya ya raia na mashirika ya Iran ambayo yameongezwa kwenye orodha ya vikwazo ya Marekani, serikali ya nchi hiyo kwa mara nyingine tena imeakhirisha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa siku nyingine 120.
Hatua hiyo kwa upande mmoja inaongeza majina ya raia na mashirika ya Kiirani yatakayowekwa kwenye orodha iliyotajwa na wakati huohuo kuilazimisha Marekani kufungamana na ahadi ilizotoa kuhusu mapatano ya nyuklia kati ya Iran na nchi sita kubwa za dunia ikiwemo Marekani yenyewe, mazungumzo yanayojulikana kwa ufupisho wa JCPOA. Hata hivyo Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesisitiza kwamba hatua hiyo haipaswi kuchukuliwa kuwa ni alama ya serikali ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kubadili msimamo wake kuhusiana na mapatano hayo ya nyuklia. Katika miezi ya hivi karibuni serikali ya Trump imekuwa na msimamo unaogongana kuhusiana na mapatano hayo.
Viongozi wa serikali hiyo akiwemo Trump mwenyewe pamoja na Nikki Haley, mwakilishi wake wa kudumu katika Umoja wa Mataifa, licha ya kudai kuwa Iran imekiuka moyo wa mapatano ya JCPOA na hivyo kusisitiza udharura wa kuangaliwa upya mapatano hayo, lakini wakati huohuo serikali ya Washington imeamua kuakhirisha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa siku 120. Suala hilo linathibitisha wazi kwamba miaka miwili baada ya kuanza kutekelezwa mapatano ya JCPOA kati ya Iran na kundi la 5+1 na wakati huohuo kuthibitishwa mara kadhaa kuwa Iran imetekeleza ahadi zake zote, Marekani bado imechanganyikiwa na kushindwa kabisa kutekeleza hata moja ya ahadi muhimu ilizotoa kuhusiana na mapatano hayo ya kimataifa.
Kuchanganyikiwa huko pia kunatokana na migongano ya kisiasa inayooneka wazi ndani ya Marekani. Kuna kundi la wanasiasa nchini Marekani ambalo linadai kwamba kutokana na kuwa matarajio ya nchi hiyo ya kuiona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inabadili misimamo yake juu ya masuala kama vile makombora na siasa zake za kieneo hayajafikiwa, Washington inapasa kuendelea kupuuza mapatano ya JCPOA na hata kujitoa kwenye mapatano hayo bila kujali malalamiko na ukosoaji wa walimwengu.
Hii ni pamoja na kuwa matamshi ya kutowajibika ya Trump katika kipindi cha kampeni zake za uchaguzi na baada ya kuingia ikulu ya White House yameiweka pagumu serikali yake kuhusiana na mapatano ya JCPOA. Pamoja na hayo, kundi jingine kubwa la wanasiasa na wataalamu wa Marekani linaamini kwamba ni vigumu kuendelea kutoa madai kuwa Iran imekiuka mapatano hayo au kutotekeleza ahadi zake katika hali ambayo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA daima umekuwa ukitoa ripoti zinazothibitisha kwamba Iran imefungamana na kutekeleza kikamilifu ahadi zake zote kuhusu mapatano hayo ya kimataifa.
Hii ni pamoja na kuwa uungaji mkono mkubwa wa karibu pande zote za Ulaya, Russia, China na Umoja wa Mataifa kwa mapatano hayo unaendelea kuisukuma nchi hiyo katika ukingo wa kutengwa kisiasa kimataifa. Kwa msingi huo licha ya kundi hilo kuendelea kuituhumu Iran juu ya masuala yasiyohusiana na Mapatano ya JCPOA lakini linaitaka serikali ya Washington kuheshimu mapatano hayo. Kwa kuzingatia suala hilo, serikali hiyo imeamua kuakhirisha vikwazo vya nyuklia kwa kipindi kingine cha siku 120 ili kuliridhisha kundi la pili na wakati huohuo kuongeza majina ya raia na mashirika mapya ya Iran kwenye orodha ya vikwazo vyake vingine ili kuliridhisha kundi la kwanza; suala ambalo linabainisha wazi kuchanganyikiwa kwa Wamarekani kuhusiana na Iran.
No comments:
Post a Comment