Uturuki imemuita balozi wa Ujerumani nchini humo jana Jumamosi(16.09.2017) kuhusiana na kile ilichosema ni mkutano wa wanamgambo wa Kikurdi mjini Kolon, wizara ya mambo ya kigeni imesema.
Wizara ya mambo ya kigeni imeeleza hayo katika taarifa inayoashiria kuchafuka zaidi kwa uhusiano kati ya mataifa hayo washirika wa NATO.
"Tunashutumu kufanyika kwa mkutano katika mji wa Kolon nchini Ujerumani wa kundi la kigaidi la PKK, na kuruhusu propaganda za kigaidi.
Tumeeleza hisia zetu kwa nguvu kabisa kwa balozi wa Ujerumani mjini Ankara, ambae aliitwa katika wizara ya mambo ya kigeni," taarifa ilisema.
Taarifa hiyo ilionekana kuzungumzia kuhusu maandamano ya Septemba 3 wakati kiasi ya Wakurdi 25,000 waliandamana mjini Kolon dhidi ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, baadhi wakibeba mabango yenye picha ya Abdullah Ocalan, kiongozi wa chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi, PKK, ambacho kimeorodheshwa kama kundi la kigaidi na Umoja wa Ulaya na Marekani, na kimepigwa marufuku nchini Ujerumani.
Uturuki imekuwa ikiishutumu Ujerumani kwa kutofanya vya kutosha kuzuwia wanaharakati wa PKK.
Watu 14,000 walishiriki katika sherehe za kitamaduni za Wakurdi, ambazo zilichukua kauli mbiu ya "Uhuru kwa Ocalan, mamlaka kwa Wakurdi," kituo cha televisheni cha WDR kimeripoti.
Kauli mbiu za PKK
Kauli mbiu hiyo inamuhusisha Abdullah Ocalan , kiongozi aliyeko kifungoni wa chama kilichopigwa marufuku cha Wafanyakazi wa Kikurdi PKK, kundi lililoorodheshwa kuwa ni kundi la kigaidi nchini Uturuki na Umoja wa Ulaya. Majeshi ya Uturuki yamo katika mzozo wa muda mrefu na kundi la PKK upande wa kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani haikujibu ombi la shirika la habari la dpa kutaka kuzungumzia hatua iliyochukuliwa na Uturuki kumuita balozi wa Ujerumani. Katika taarifa iliyotolewa jana Jumamosi , wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki lisema inashutumu tukio la mjini Kolon, na kudai kwamba "propaganda ya ugaidi ilifanyika katika tukio hilo na kundi lenye mahusiano na kundi la kigaidi la PKK nchini Ujerumani, na kwamba picha za Ocalan zilioneshwa, kitu ambacho ni kinyume na sheria.
Gazeti la mjini Kolon la Express limeripoti kwamba kabla ya maandamano kuanza polisi mwanamke mwenye umri wa miaka 24 alipata majeraha kichwani na alilazimika kupelekwa hospitali. Polisi pia walikamata bendera na kutoa onyo rasmi kwa washiriki , Express lilisema.
Hii ni mara ya pili mwaka huu ambapo Uturuki ilimwita balozi wa Ujerumani nchini humo kuhusiana na maandamano ya Wakurdi nchini Ujerumani.
Baada ya maandamano ya mamia kwa maelfu ya Wakurdi mjini Frankfurt mwezi Machi, polisi ilifanya uchunguzi. Walisema katika wakati huo hawakuingilia maandamano hayo ili kuepusha kuchochea ghasia.
Wakurdi ni asilimia 15 ya idadi ya watu nchini Uturuki na mara kadhaa hushutumu kile wanachokiona kuwa ni ubaguzi unaofanywa na serikali. Chama cha PKK , ambacho kimekuwa kikipigana na serikali ya Uturuki kwa zaidi ya miaka 30, kimeelezwa kuwa ni kundi la kigaidi nchini Ujerumani tangu mwaka 1993.
No comments:
Post a Comment