Wednesday, September 13, 2017

AYATULLAH MAKARIM SHIRAZI; NCHI ZA KIISLAMU ZIFUATILIYE MAUAJI YA WAISLAMU WA MYANMAR

Ayatullah Nasir Makarim Shirazi, mmoja wa Marjaa-Taqlidi wa hapa nchini ameeleza kusikitishwa na kimya cha Umoja wa Mataifa kuhusiana na mauaji ya Waislamu wa Myanmar na kusisitiza kwamba inapasa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiislamu waitishe kikao cha haraka ili kusimamisha mauaji ya Waislamu hao madhulumu.
Akizungumza leo wakati wa darsa ya masomo ya juu kabisa ya fiqhi huko Qum kusini mwa Tehran, Ayatullah Makarim Shirazi ameongeza kuwa serikali ya Myanmar inapaswa iitishe kikao na maulamaa wa nchi za Kiislamu na kueleza sababu za mauaji ya kimbari yanayofanywa dhidi ya Waislamu.
Hapo jana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei naye pia alikosoa kimya cha jumuiya za kimataifa na wanaojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu kuhusiana na matukio ya maafa ya Myanmar na kusisitiza kwamba njia ya utatuzi wa kadhia ya Myanmar ni kuchukuliwa hatua za kivitendo na nchi za Kiislamu na kuishinikiza kisiasa na kiuchumi serikali isiyo na huruma ya nchi hiyo.
Waislamu madhulumu wa Myanmar
Wakati huohuo Ibrahim Rahimpour, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na eneo la Asia na Oceania ametangaza leo kuwa misaada ya kibinadamu ya Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya Waislamu wa Myanmar itapelekwa nchini Bangladesh siku ya Ijumaa.
Akizungumza katika kikao cha dharura cha Kamati ya Bunge ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje Rahimpour ameongeza kuwa tani 100 za misaada ya kibinadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikijumuisha vifaa vya hospitali na madaktari bingwa kadhaa zitatumwa kwa ajili ya kuwasaidia Waislamu wa Myanmar.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua kwamba, mbali na hatua hiyo, mashauriano ya kisiasa yanaendelea kufanywa na serikali ya Myanmar na nchi jirani na nchi hiyo ili kuzuia mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu.
Wimbi jipya la mauaji ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar lilianza tarehe 25 Agosti mwaka huu. Hadi hivi sasa maelfu ya Waislamu hao wameshauawa na kujeruhiwa na wengine karibu laki tatu wamekimbia makazi yao.../

No comments:

Post a Comment