Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF)
umetangaza kuwa, karibu asilimia 60 ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya
Rohingya waliokimbilia Bangladesh kutokana na mauaji na ukatili
unaofanywa na Mabudha na jeshi la Myanmar, ni watoto wadogo.
UNICEF imetangaza kuwa, hadi sasa watoto 1400 wa Waislamu wa
Rohingya wamesajiliwa baada ya kuvuka mpaka na kuingia Bangladesh wakiwa
peke yao bila ya wazazi au wasimamizi wao.
Taarifa ya UNICEF imesema kuwa, watoto hao wakimbizi wameshuhudia kwa
macho mauaji ya wazazi na watu wa familia zao au kuchomwa moto makazi
na nyumba zao.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kambi za wakimbizi za Waislamu wa
Rohingya nchini Bangladesh zina hali mbaya sana na kwamba makumi ya
maelfu ya wakimbizi hao wanaoshi katika maeneo yasiyo na usalama na
yasiyofaa kwa ajili ya watoto.
Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuawa katika mashambulizi
yanayoendelea kufanywa na Jeshi la Myanmar na Mabudha wenye misimamo ya
kuchupa mipaka hususan katika jimbo la Rakhine.
No comments:
Post a Comment