Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran
amesema kuwa hotuba iliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani katika
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni ya kipumbavu na kwamba Trump ni mtu
mwenye akili finyu, kidhambi na mpenda vita.
Katika hutuba yake ya hivi karibuni kwenye Baraza Kuu la Umoja
wa Mataifa, Rais huyo wa Marekani aliituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
ambayo ni miongoni mwa mihimili na nguzo kuu za kupambana na magaidi
katika eneo la Mashariki ya Kati, kuwa inaunga mkono ugaidi.
Katika hotuba zake za leo kwenye Swala ya Ijumaa, Hujjatul Islam
Walmuslimin Kazem Seddiqi amesema matamshi yasiyo ya kidiplomasia ya
Trump ni kielelezo cha hasira na kuchanganyikiwa.
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria kufeli kwa njama za
Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema: Katika miezi ya
hivi karibuni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wapiganaji wa Hizbullah na
Russia wametoa kipigo kikali kwa magaidi wanaoungwa mkono na kusaidiwa
na Marekani na washirika wake.
Hujjatul Islam Walmuslimin Seddiqi ameongeza kuwa, Daesh, al
Qaida, Taliban na magenge mengine kadhaa ya kigaidi ni watoto wa
Marekani na Saudi Arabia na kusisitiza kuwa: Nchi hizo mbili zimetumia
mamilioni ya fedha za watu wao kwa ajili ya kuanzisha makundi kama hayo
ya kigaidi. Amesema, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni mapinduzi ya watu
waliodhulumiwa kote duniani na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu daima
itaendelea kuwasaidia watu wa Iraq na Syria katika vita vyao dhidi ya
magaidi.
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran pia amewapa mkono wa pole
Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa kuwadia mwezi wa Muharram na
kusisitzia kuwa, Imam Hussein bin Ali (as) aliuawa katika mwezi huu
katika mapambano yake dhidi ya mfumo na utawala wa kidhalimu na
kibeberu.
No comments:
Post a Comment