Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini
amejibu matamshi ya vitisho ya Rais Donald Trump wa Marekani na kusema
kuwa, rais huyo wa Marekani ana matatizo ya kiakili na kwamba atalipa
gharama ya matamshi yake ya vitisho dhidi ya Pyongyang.
Katika sehemu nyingine, kiongozi
huyo wa Korea Kaskazini sambamba na kuashiria matamshi ya hivi karibuni
ya rais wa Marekani aliyetishia kuishambulia Pyongyang amesema kuwa,
nitamfanya kiongozi huyo wa Marekani ajutie matamshi yake aliyoyatoa
katika mkutano mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kwa
kuitishia Korea Kaskazini.
Itakumbukwa kuwa Jumatatu iliyopita
katika mkutano huo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Trump
alizishambulia nchi kadhaa za dunia na kutoa vitisho dhidi ya nchi hizo
badala ya kuzungumzia amani na usalama. Akiizungumzia Korea Kaskazini
Trump alisema, Marekani italazimika kuiangamiza kikamilifu nchi hiyo ya
Asia, isipokuwa kama Pyongyang itakubali kurudi nyuma kuhusiana na
miradi yake ya silaha za nyuklia. Kadhalika rais huyo wa Marekani ambaye
hadi sasa ameendelea kukosolewa duniani kutokana na matamshi yake
yasiyo ya mantiki, alimtaja Kim Jong-un kwa jina la 'Mtu wa Makombora'
na kuongeza kuwa, kiongozi huyo wa Korea Kaskazini anafanya mambo
yatakayopelekea yeye, mfumo na raia wa nchi yake kujiangamiza.
Kama hiyo haitoshi usiku wa Alkhamisi ya
jana Trump alisaini dikrii mpya ambayo inaitaka Wizara ya Hazina ya
Marekani kuwawekea vikwazo watu au taasisi za kigeni zinazoshirikiana
kibiashara na Korea Kaskazini. Kabla ya hapo pia Korea Kaskazini
iliwekewa vikwazo vipya na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
kutokana na kuyafanyia majaribio makombora yake ya balestiki na silaha
za nyuklia. Pyongyang imekuwa ikisisitiza kuwa, itaendelea kujiimarisha
kijeshi ili kukabiliana na chokochoko za Marekani na washirika wake
dhidi yake.
No comments:
Post a Comment