Wednesday, September 13, 2017

KUENDELEA KUKOSOLEWA SIASA TRUMP KUHUSIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Katika hali ambayo kimbunga cha Irma bado kinaendelea kuyakumba maeneo kadhaa ya Marekani, baadhi ya duru za kisiasa na vyombo vya habari nchini humo vimeonyesha wasi wasi wao kuhusiana na siasa za Rais Donald Trump katika uwanja wa mabadiliko ya tabianchi.
John McCain, seneta wa chama cha Republican amekosoa vikali msimamo wa Rais Donald Trump kuhusiana na suala hilo. Akizungumza katika mahojiano maalumu, McCain amesema kuwa, hivi sasa dunia inashuhudiwa mabadiliko ya hali ya hewa ambayo hayajawahi kushuhudiwa huko nyuma. Amesisitizia umuhimu wa kutumiwa nyuklia kama chanzo salama cha nishati safi kuliko siasa za Trump, zinazosisitiza juu ya utumiwaji wa nishati ya mafuta.
John McCain
Amesema kuwa, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuna udharura wa kuchukuliwa hatua ambazo hazitowadhuru raia wa kawaida. Matamshi ya John McCain yametolewa katika hali ambayo katika wiki mbili zilizopita Marekani imekuwa ikishuhudia vimbunga vikali cha hivi karibuni zaidi kikiwa ni kimbunga cha Irma katika jimbo la Florida ambacho kimesababisha uharibifu mkubwa jimboni humo. Kabla ya hapo pia yaani mwezi Agosti, wakazi wa majimbo ya Texas na Louisiana walishuhudia kimbunga kingine cha Harvey ambapo sambamba na kusababisha uharibifu mkubwa unaokadiriwa kuwa wa dola bilioni 180, zaidi ya watu 60 walipoteza maisha katika kimbunga hicho. Ripoti iliyotolewa na serikali ya Washington inaonyesha kwamba, mabadiliko ya tabianchi yanayoshuhudiwa duniani hivi sasa, yanaufanya mwaka jana wa 2016 kuwa mwaka uliokuwa na joto jingi zaidi katika miongo kadhaa ya hivi karibuni. Wataalamu wa mambo wameonya kwamba, hatua ya Marekani kujiondoa katika mkataba wa kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa wa mjini Paris, Ufaransa, inaweza kusababisha ongezeko kubwa la joto na uharibifu wa hali ya hewa duniani.
Rais  Donald Trump wa Marekani
Pamoja na hayo, lakini bado Rais Donald Trump anaendelea kupuuza suala la mabadiliko ya tabianchi ambapo sambamba na kufumbia macho indhari za wataalamu, tarehe 20 Januari mwaka huu alitangaza kuiondoa nchi yake katika Mkataba Mazingira wa Paris. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, vimbunga vya Harvey na Irma vimeongeza mashinikizo dhidi ya serikali ya Marekani kutokana na kufumbia kwake macho tahadhari zinazotolewa juu ya taathira hasi za mabadiliko ya tabianchi. Kwa mtazamo wa weledi wa mambo, Trump hapaswi kufanya ujeuri unaompelekea kupinga uchunguzi na utafiti unaofanywa na wataalamu wa taaluma tofauti na hasa wa masuala ya mazingira. Katika uwanja huo Noam Chomsky, msomi na mkosoaji mashuhuri wa Marekani anaamini kwamba, Rais Donald Trump anakusudia kuiangamiza dunia.
Vimbunga vikali vnavyoendelea kuikumba Marekani 
Baada ya kutangazwa hali ya hatari katika jimbo la Florida, Tomás Pedro Regalado, Meya wa mji wa Miami alisema kuwa, sasa umefika wakati wa kufanya uchunguzi na mazungumzo kuhusiana na suala zima la tabianchi na Trump kwa kushirikiana na Wakala wa Kulinda Mazingira wa nchi hiyo ili kuchukua maamuzi muhimu kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa. Hata kama hadi sasa haijafahamika wazi ikiwa ni mabadiliko ya tabianchi ndiyo yamepelekea kuongezeka vimbunga vya mwaka 2017 nchini Marekani na katika maeneo mengine ya duania au la, lakini wataalamu wa mambo wanaamini kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwamba vimbunga hivyo huenda vikawa vimeathiriwa moja kwa moja na mabaliko ya hali ya hewa duniani. Ukweli ni kwamba, ikiwa Rais Donald Trump na serikali yake wataendelea kupinga ukweli kwamba mabadiliko ya tabianchi na taathira zake ndicho chanzo cha vimbunga vinavyoshuhudiwa hii leo, basi maisha ya mamilioni ya Wamarekani yatakuwa katika hatari kubwa.

No comments:

Post a Comment