Friday, September 22, 2017

KAMANDA SALAMI: KUINGIA VITANI NA IRAN HAKUTAKUWA NA MATOKEO GHAIRI YA KUSHINDWA

Kamanda Salami: Kuingia vitani na Iran hakutakuwa na matokeo ghairi ya kushindwa
Naibu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (SEPAH) sambamba na kusisitiza kuwa kuingia vitani na Iran hakuwezi kuwa na natija nyinginge ghairi ya kushindwa amesema kuwa Wiki ya Kujilinda Kutakatifu imeleta izza ya usalama kwa taifa hili.
Brigedia Jenerali Hussein Salami ameyasema hayo leo katika mji wa Gorgab wa mkoa wa Isfahan, katikati mwa Iran na kuongeza kuwa, kujilinda kutakatifu ni alama ya umoja wa taifa la Iran mkabala wa uistikbari wa dunia. Akibainisha kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imerithi utamaduni wa tukio la Ashura amesema kuwa, kile kinacholifanya taifa hili kuendelea kusimama imara dhidi ya Marekani, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na washirika wao ni uimara na ushujaa wa wanaume na wanawake wa Iran walikokurithi kutoka utamaduni wa Ashura na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. 
Brigedia Jenerali Hussein Salami
Naibu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (SEPAH) amesema kuwa katika kipindi cha miaka minane ya kujitetea kutakatifu Iran ya Kiislamu ikiwa peke yake iliweza kuonyesha adhama yake mbele ya mabeberu wa dunia na kwamba baraka za kujitolea muhanga wanamapambano wa vita hivyo, ndiko kulikoliletea taifa la Iran ushujaa na uimara. Aidha ameashiria matamshi yasiyo ya kidiplomasia ya Rais Donald Trump wa Marekani katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) na kuongeza kuwa, umefika wakati kwa serikali ya Washington kujiepusha na upuuzi wa namna hiyo.

No comments:

Post a Comment