Saturday, September 16, 2017

IRAN; MOJAYA MADOLA MANNE YANAYOONGOZA KATIKA TEKNOLOJIA YA SATALAITI DUNIANI

Nguvu na uwezo wa kielimu sambamba na nguvu za kiulinzi na makombora ni miongoni mwa mambo muhimu yanayojenga nguvu na uwezo wa taifa lolote katika zama hizi; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa upande wake imepiga hatua nzuri katika uga wa nguvu na uwezo wa kielimu na kisayansi hususan katika teknolojia ya satalaiti.
Mshauri wa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza siku ya Alkhamisi kuwa: Iran ni moja ya nchi nne duniani zinazoongoza katika nyanja zote za teknolojia ya satalaiti. Brigedia Jenerali Mohammad Hassan Nami amesema Iran inao utaalamu na uwezo mkubwa katika nyuga za teknolojia ya satalaiti ikiwemo vituo vya kurushia, mitambo ya kubebea angani, satalaiti zenyewe pamoja na vituo vya upokeaji na uongozaji.
Brigedia Jenerali Mohammad Hassan Nami
Mafanikio katika uga wa kutuma satalaiti angani sambamba na uwezo wa kuunda makombora ya aina mbalimbali yenye uwezo na malengo tofauti yameifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iwe na nguvu na uwezo katika nyanja za aina kwa aina. Kutengeza satalaiti na kuituma anga za mbali kwa kutumia maroketi ya kubebea satalaiti ni upeo wa juu kabisa wa utunishaji nguvu na misuli ya uwezo wa nchi yoyote ile katika uga wa teknolojia ya anga za mbali. Katika uwanja huo, Iran imetuma angani satalaiti mbalimbali kwa kutumia maroketi ya kubebea satalaiti; na hivi sasa ni miongoni mwa nchi nne zinazoongoza katika uga huo duniani ikiwa pia imo kwenye mikakati ya kutuma wanadamu katika anga za juu. Akizungumzia suala hilo, Fat-hollah Ummi, Mkuu wa kituo cha utafiti wa anga za mbali cha Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia ya Iran alitangaza wiki iliyopita kwamba: "marubani wanne wenye uzoefu mkubwa hivi sasa wanapatiwa mafunzo makubwa na magumu ili hatimaye wawili miongoni mwao wachaguliwe kwa ajili ya kutumwa kuelekea anga za mbali".
Satalaiti ya Omid iliyotumwa na Iran katika anga za mbali
Kabla ya hapo, mnamo mwaka 2013, wanasayansi wa anga za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walifanikiwa kutuma anga za mbali kima wawili waliopewa majina ya Aftab na Fargam; na kwa mujibu wa Fat-hollah Ummi hadi sasa kima hao wawili wangali hai; na wataalamu wa Kiirani wanafanya utafiti kuhusu athari za safari za anga za mbali kwa mtoto aliyezaliwa na kima hao.
Kwa kutegemea uwezo na utaalamu wake wa ndani na juhudi za waatalamu wake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kuwa moja ya mataifa yenye uwezo wa juu katika nyuga mbalimbali za teknolojia ya satalaiti. Kutokana na mafanikio makubwa iliyopata, kila pale inapotuma satalaiti kwa mafanikio kuelekea anga za mbali, maadui zake wakiongozwa na Marekani hushindwa kuvumilia jambo hilo. Kwa kutoa mfano, mnamo tarehe 27 Julai mwaka huu, Iran ilifanikiwa kurusha kwa mafanikio roketi la kubebea satalaiti la Simorgh katika kituo cha taifa cha anga za mbali cha Imam Khomeini (MA) kilichopo hapa mjini Tehran. Siku moja tu baada ya mafanikio hayo, yaani tarehe 28 Julai, Wizara ya Hazina ya Marekani ilitumia kisingizio cha kufanyiwa jaribio roketi la Simorgh ambalo lilihusu masuala ya utafiti tu na kisayansi, kuzijumuisha taasisi sita za Iran kwenye orodha ya vikwazo vyake dhidi ya taifa hili. Katika hatua nyengine inayofanana na hiyo, Alkhamisi ya tarehe 14 ya mwezi huu wa Septemba wizara hiyo iliongeza majina ya watu na mashirika mengine kadhaa ya Kiirani yanayohusika na masuala ya makombora kwenye orodha ya vikwazo dhidi ya Iran. Hatua hiyo ya serikali ya Washington inakinzana na sheria za kimataifa na hata makubaliano ya nyuklia na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Akizungumza siku tatu zilizopita pembeni ya mkutano wake na Katibu Mkuu wa Shirikia la Ushirkiano wa anga za mbali la Asia na Oceania (APSCO), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia za Mawasiliano wa Iran Mohammad Javad Azari Jahrami alisema: "Sekta ya anga za mbali haikuashiriwa kwa namna yoyote ile kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na hata katika azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama pia sekta ya satalaiti ya Iran haijawekewa mpaka wowote".
Rais Hassan Rouhani alipokagua uundaji wa roketi la Simorgh
Shughuli za satalaiti na utumaji wake kuelekea anga za mbali kwa malengo ya utafiti ni jambo la dharura na la kawaida kwa nchi yoyote ile. Kwa sababu hiyo, bila kujali hatua za kutapatapa zinazochukuliwa na Marekani, Iran ingali inaendelea kupiga hatua na kusonga mbele katika uga huo ambapo hivi sasa inajiandaa kutuma anga za mbali satalaiti nyengine mpya iliyopewa jina la "Satalaiti ya Urafiki". Kuwa na nguvu na uwezo katika sekta mbalimbali kumeifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iwe dola athirifu na lenye sauti katika eneo na ulimwenguni kwa jumla, ambapo licha ya kuandamwa na mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi hivi sasa imekuwa moja ya madola yanayoongoza katika uga wa utaalamu wa makombora na satalaiti duniani.../

No comments:

Post a Comment