Wananchi wa Afrika Kusini wamefanya maandamano wakilaani mauaji ya kimbari yanayofanyika nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Waandamanaji hao waliokusanyika mbele ya ubalozi wa Myanmar mjini Pretoria walikuwa wakipinga nara za kutaka kukomeshwa mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
Maulana Bham ambaye ni mjumbe wa Baraza la Waislamu nchini Afrika Kusini alisema katika maandamano hayo kwamba, walimwengu wanapaswa kuchukua hatua dhidi ya mauaji ya umati yanayofanyika dhidi ya Waislamu nchini Myanmar.
Mauaji yanayofanywa na Mabudha wa Myanmar wakishirikiana na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya yameamsha hasira na malalamiko katika nchi mbalimbali duniani.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya Waislamu laki nne wa Rohingya wamelazimishwa kuhama makazi yao na kukimbilia Bangladesh tangu tarehe 25 mwezi uliopita wa Agosti kutokana na ukatili na mauaji yanayofanywa na Mabudha. Waislamu wengine zaidi ya elfu sita wameuawa na wengine elfu 8 wamejeruhiwa.
Ukatili mkubwa zaidi dhidi ya Waislamu nchini Myanmar unafanyika katika mkoa wa Rakhine ulioko magharibi mwa nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment