Wednesday, January 18, 2017

WHITE HOUSE YAKIRI, OBAMA AMESHINDWA KUFUNGA GEREZA LA GUANTANAMO

Ikulu ya Marekani White House imekiri kuwa Rais Barack Obama wa nchi hiyo ameshindwa kufunga gereza la kutisha la Guantanamo mwishoni mwa muhula wake huu wa pili kama alivyoahidi.
Josh Earnest, Katibu wa masuala ya vyombo vya habari wa White House amesema: "Kwa sasa sidhani kama tunaweza kutekeleza lengo letu la kufunga jela ya Guantanamo kama ilivyotazamiwa."
Ameongeza kuwa, wanasiasa wa mirengo yote katika Bunge la Kongresi la nchi hiyo walilitumia suala la kufungwa Guantanamo kama wenzo la kisiasa na ni kwa sababu hiyo ndipo sasa serikali ya Rais Obama imeshindwa kutekeleza ahadi hii.
Josh Earnest, Katibu wa masuala ya vyombo vya habari wa White House
Hii ni katika hali ambayo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) hivi karibuni iliwahamisha wafungwa 15 wa jela hiyo ya kutisha ya Guantanamo na kuwapeleka katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) huku 10 wakipelekwa Oman, huu ukiwa ni uhamisho mkubwa zaidi wa wafungwa hao kufanywa na utawala wa Rais Barack Obama wa Marekani.
Mapema mwezi huu, Rais mteule wa Marekani Donald Trump alimuonya rais anayeondoka wa nchi hiyo Barack Obama juu ya kuwahamisha wafungwa wa jela ya Guantanamo iliyoko nchini Cuba. Trump aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: "Hakuna kuwahamisha wafungwa zaidi wa Gitmo, hawa ni watu hatari ambao hawafai kuachwa warejee katika uwanja wa mapambano."
Rais Barack Obama Januari mwaka 2009 aliahidi baada ya kushinda uchaguzi kuwa, katika muda wa mwaka mmoja angeifunga jela ya Guantanamo, ahadi ambayo ameshindwa kuitekeleza hadi sasa ambapo anaondoka madarakani.
Jela ya kijeshi ya Marekani katika ghuba ya Guantanamo nchini Cuba

No comments:

Post a Comment