Monday, January 2, 2017

MWAKA MMOJA TANGU SAUDIA IMUUWE KIKATILI MTETEZI WA HAKI ZA BINADAMU SHEIKH NIMR AL NIMR

Leo tarehe Pili Januari umetimia mwaka mmoja tangu utawala wa kifalme wa Saudi Arabia umuue kikatili mwanazuoni mashuhuri na mtetezi mkubwa wa haki za binadamu nchini humo Sheikh Nimr Baqir al Nimr.
Kwa mnasaba huo wapinzani wa utawala wa Kifalme wa Saudia wamefanya maandamano katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo na katika miji kadhaa ya nchi za kigeni huku wadau wa mitandao ya kijamii wakilaani na kumkumbuka msomi huyo aliyesimama kidete kupigania haki za wanaodhulimiwa.
Sheikh Baqir al Nimr alikamatwa na vyombo vya usalama vya Saudi Arabia Julai mwaka 2012 kufuatia maandamano makubwa yaliyofanyika Februari 2011 katika eneo lenye Waislamu wengi zaidi wa madhehebu ya Shia la Qatif huko mashariki mwa Saudia. Tarehe 15 Oktoba 2015 Mahakama ya utawala wa Aal Saud ilimhukumu kifo mwanazuoni huyo wa Kiislamu kwa tuhuma zisizo na msingi eti za kuhujumu usalama wa taifa na hatimaye msomi huyo aliuawa kwa kukatwa kichwa na mwili wake ukasulubiwa.

Sheikh Baqir Nimr
Mauaji ya Sheikh Baqir al Nimr ambayo yalitambuliwa kuwa ni jinai ya kutisha na ugaidi wa kiserikali, yalilaaniwa sana na jumuiya za kikanda na kimataifa za kutetea haki za binadamu. Ili kuficha na kutaka kuhalalisha mauaji ya mwanamapambano huyo, utawala wa Saudi Arabia pia uliwanyonga na kuwaua vijana kadhaa pamoja na Sheikh Nimr ambao walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za ugaidi.
Mbinyo na ukandamizaji wa serikali ya Saudia dhidi wananchi hususan Waislamu wa madhehebu ya Shia, unaongezeka siku baada ya siku na askari usalama wa nchi hiyo wamezidisha mashambulizi dhidi ya wakazi wa maeneo ya mashariki. Kwa vyovyote vile, hali ya Saudia na malalamiko yanayoongezeka kila uchao ya wananchi dhidi ya watawala na jinai zinazofanywa na Aal Saud hususan mauaji ya Sheikh Nimr, ni miongoni mwa makosa ya kistratejia ya utawala huo ambayo taathira zake zimezidisha matatizo ya utawala huo wa kifalme na kutikisa nguzo zake.

Wasaudia wakiandamana kulaani mauaji ya Sheikh Nimr
Duru za kisheria pia zimekuwa zikilaani mauaji ya mpigania haki huyo mashuhuri na kusisitiza kuwa, msomi huyo aliuawa kwa sababu tu ya kukosoa utawala wa Saudia na kupinga dhulma na ukandamizaji, jambo ambalo si kosa la kumfanya mtu auawe kwa kukatwa kichwa. Wadadisi wa mambo wanasema, utawala wa Saudia unatumia hukumu za kifo na kukata watu vichwa kama wenzo wa kunyamazisha wapinzani wake na kujenga mazingira ya hofu ili kuwatisha na kuwazua wapinzani kukosoa utendaji na dhulma za utawala huo. Hata hivyo na licha ya ukandamizaji huo dhidi ya wapinzani, maandamano na malalamiko dhidi ya Aal Saudi yamekuwa yakishadidi siku baada ya siku. Suala hili linaonesha kuwa, mbinu za kujenga mazingira ya hofu na ukandamizaji zimeshindwa kuwanyamazisha wapinzani na harakati ya mwamko wa wananchi huko Saudi Arabia. 

Image Caption
Kwa hakika damu ya mpigania haki na uadilifu huyo imezidisha mori na vuguvugu la mwamko la watu dhidi ya ukandamizaji wa Saudi Arabia na hapana shaka kuwa Sheikh Nimr Baqir al Nimr ataendelea kukumbukwa katika harakati zote za kudai haki na kupinga dhulma na ukatili wa watawala wa Aal Saud.

No comments:

Post a Comment