Monday, January 2, 2017

TUNISIA KATIKA MTANZIKO WA KIUSALAMA, MAGAIDI EIFU TATU WAPO NJE YA NCHI

Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia tarehe 31 mwezi Disemba mwaka jana alieleza kuwa magaidi elfu tatu raia wa Tunisia wametapakaa katika pembe mbalimbali za dunia khususan huko Iraq, Syria na Libya.
Beji Caid Essebsi aliongeza kuwa baadhi ya ripoti zinasema kuna jumla ya magaidi elfu kumi wa Tunisia lakini takwimu hizo si sahihi na kuwa magaidi raia wa Tunisia walioko Iraq, Syria, Libya, Yemen na Afrika idadi yao ni 2926.
Tunisia ni nchi pekee ya Kiarabu ambayo imeweza kuvuka kwa mafanikio kipindi cha mpito baada ya mageuzi  na mapinduzi ya wananchi mwaka 2011. Kwa kutambua hali ya mambo na uzoefu wa migogoro ya Misri, Libya na Yemen, vyama, makundi ya kisiasa na shakhsia wa Tunisia waliweza kuvuka kipindi cha mpito kwa maafa na hasara za kiwango cha chini. Katika kipindi cha miaka sita ya hivi karibuni, Tunisia haikukabiliwa na vitisho vingi vya usalama ikilinganishwa na nchi tatu za Libya, Yemen na Misri na tishio kuu zaidi ambalo limekuwa likiitatiza nchi hiyo ni matatizo ya kiuchumi. Pamoja na hayo imejikuta ikihusika bila ya kutaka na machafuko na migogoro inayozikabili nchi nyingine za Kiarabu na raia wengi wa nchi hiyo hususan tabaka la vijana wamejiunga na makundi ya kigaidi katika nchi za Syria, Iraq, Libya na Yemen. Kwa sasa makundi ya kigaidi yamedhoofika sana hususan huko Syria na Iraq, na uwezekano wa kurejea nchini karibu magaidi elfu tatu raia wa Tunisia limegeuka na kuwa changamoto kubwa ya kiusalama kwa nchi hiyo.
Magaidi wa kitakfiri wa Daesh ambao ndani yake kuna raia wa nchi mbalimbali wakiwemo vijana wa Tunisia
Baadhi ya vyama vya siasa nchini Tunisia kikiwemo chama cha Nidaa Tounes cha Rais Beji Caid Essebsi vinaamini kuwa, kurejea nchini magaidi hao ni tishio kubwa kwa usalama wa Tunisia. Chama cha Nidaa Tounes kinapinga suala la kurejea nchini magaidi hao. Hata hivyo baadhi ya wanachama wa chama cha An Nahdha katika Bunge la taifa wanaamini kuwa, magaidi ambao ni raia wa Tunisia wana haki ya kurudi nchini kwa sababu wao ni raia wa nchi hiyo. Wakati huo huo wananchi wa Tunisia wamekuwa wakifanya maandamano na kutangaza upinzani wao dhidi ya suala la kurejea nchini magaidi hao.  
Wananchi wa Tunisia wakiandamana kupinga kurejea magaidi wa Daesh nchini humo 
Licha ya baadhi ya wanachama wa chama cha Nidaa Tounes kupinga jambo hilo, lakini Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia ametangaza rasmi kuwa, haiwezekani kuwazuia magaidi hao kurejea nyumbani kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo. Essebsi amesema kuwa iwapo wananchi wote watapinga suala la kurejea magaidi nchini, basi katiba itafanyiwa marekebebisho.
Msimamo huo rasmi wa Rais wa Tunisia unaonyesha kuwa, magaidi waliotajwa hatimaye watarejea nchini humo. Kurejea magaidi hao kunaweza kuharibu matunda ya mapinduzi ya nchi hiyo ya mwaka 2011 na kuzidisha pia tisho la ugaidi kwenye orodha ndefu ya matatizo ya kiuchumi na kiusalama ya Tunisia. 

No comments:

Post a Comment