Wednesday, January 4, 2017

JESHI LA GAMBIA LATANGAZA KUMUUNGA MKONO RAIS YAHYA JAMMEH

Kamanda wa Jeshi la Gambia ametoa ujumbe akitangaza uungaji mkono kamili wa jeshi la nchi hiyo kwa Rais Yahya Jammeh ambaye amekataa kukabidhi madaraka ya nchi kwa njia ya amani baada ya kushindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo mwezi uliopita.
Taarifa hiyo imetangazwa na Jenerali Othman Badjie na kumuunga mkono kiongozi huyo aliyeko kwenye mashinikizo makubwa ya kikanda ya kimataifa yanayomtaka akabidhi madaraka kwa rais mteule wa Gambia, Adama Barrow. 
Rais Yahya Jammeh ambaye amekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 22 alishindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka jana na kukubali matokeo yaliyompa ushindi hasimu wake Adama Barrow. Hata hivyo siku chache baadaye aliibuka na kutilia shaka matokeo hayo sanjari na kukataa kuondoka madarakani.
Viongozi wa Ecowasi wamemtaka Jammeh ang'atuke madarakani
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) imetishia kutuma vikosi vya kieneo nchini Gambia, iwapo Rais Yahya Jammeh atakataa kukabidhi madaraka wakati muda wake utakapiomalizika rasmi Januari 19 mwaka huu.
Jammeh amekataa kukabidhi madaraka kwa rais mteule akidai kuwa zoezi la uchaguzi wa mwezi uliopita nchini Gambia lilitawaliwa na dosari nyingi na anataka uchaguzi wa rais ufanyike tena.

No comments:

Post a Comment