Friday, January 20, 2017

BARROW: YAHYA JAMMEH AMEKUBALI KUONDOKA MADARAKANI GAMBIA

Rais Yahya Jammeh wa Gambia amekubali kuondoka madarakani kumpisha rais mpya Adama Barrow.
Kwa mujibu wa ripoti,  Jammeh anaondoka nchini humo kwenda kuishi uhamishoni, ingawa bado haijafahamika ni nchi gani ataelekea. Habari za kuondoka rais huyo aliyetawala Gambia kwa miaka 22 sasa zimetolewa na rais anayetambuliwa na jamii ya kimataifa Adama Barrow kupitia mtandao wake wa Twitter. Barrow ameeleza hayo baada ya mazungumzo ya saa kadha yaliyokusudia kumshawishi Yahya Jammeh kukubali matokeo ya uchaguzi wa tarehe Mosi Disemba mwaka jana.
Aliyekuwa rais wa Gambia Yahya Jammeh
Hii ni katika hali ambayo nchi kadhaa za Afrika Magharibi zimewatuma wanajeshi wao nchini Gambia na kutishia kumuondoa Jammeh madarakani kwa nguvu iwapo angekaidi amri ya kuachia madaraka kwa hiari. Barrow amekuwa nchini Senegal kwa takriban wiki moja sasa ambapo pia aliapishwa kuwa rais mpya wa Gambia katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Dakar Alkhamisi iliyopita. Sasa Barrow anatambuliwa na jamii ya kimataifa kuwa kiongozi mpya wa Gambia.

No comments:

Post a Comment