Sunday, January 1, 2017

MWAKA MPYA WA 2017 NACHANGAMOTO ZINAZOUKABILI ULIMWENGU

Mwaka mpya wa 2017 umeanza leo sambamba na shambulizi lililofanyika katika klabalu moja ya starehe mjini Istanbul huko Uturuki na kuua watu karibu 40 na kujeruhiwa makumi ya wengine.
Tukio hilo ni ishara kwamba mwaka mpya wa 2017 huwenda ukatawaliwa na machafuko na umwagaji damu zaidi ya miaka iliyopita.
Ugaidi ambao katika miaka hii ya sasa umekuwa zimwi kubwa linalovuruga usingizi na usalama wa walimwengu kutokana na kupuuzwa vyanzo na sababu zake halisi na vilevile kutumiwa vibaya na baadhi ya nchi kwa malengo ya kisiasa, sasa umepanua mbawa zake katika maeneo mbalimbali ya dunia. Inaonekana zimwi hilo la ugaidi litatafuna idadi kubwa zaidi ya wanadamu katika mwaka huu wa 2017 na kuenea katika maeneo mengine ya dunia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kushindwa mtawalia kundi la Daesh na magaidi wengine katika nchi za Syria na Iraq kumewafanya wanachama wa makundi hayo warejee katika nchi zao huko Ulaya, Marekani na kaskazini mwa Afrika, suala ambalo ni hatari kubwa kwa maisha ya watu, usalama na amani ya nchi hizo. 
Wapiganaji wa kundi la Daesh
Hata hivyo inatupasa kuelewa kuwa, ugaidi sio changamoto kubwa pekee inayoikabili dunia katika mwaka huu mpya wa 2017. Hitilafu za kisiasa kati ya nchi zenye taathira katika mfumo wa kimataifa zinaweza kuyafanya maisha ya mamilioni ya wanadamu kuwa yenye mashaka makubwa. Kwa mfano tu tunaweza kuashiria hitilafu zilizopo baina ya rais mteule wa Marekani, Donald Trump na nchi za Ulaya kuhusu makubaliano ya hali ya hewa ya Paris. Hii ni kwa sababu, iwapo Trump ataiondoa Marekani katika makubaliano hayo ya Paris kama alivyoahidi, basi hapana shaka kwamba, ulimwengu utakabiliwa na uchafuzi mkubwa zaidi wa mazingira na wakati huo mabadiliko ya hali ya hewa yatakuwa na taathira kubwa zaidi kwa maisha ya wanadamu. 
Donald Trump
Katika upande mwingine kuchaguliwa Donald Trump kuwa rais wa Marekani kumezidisha wasiwasi kuhusu ushindani wa kibiashara kati ya madola mkubwa kiuchumi duniani. Iwapo Marekani na China zitazidisha ushindani mpana juu ya masuala ya kibiashara, basi uchumi dhaifu wa dunia utakumbwa na mashinikizo zaidi na hatimaye wahasirika wakubwa watakuwa nchi dhaifu na mamilioni ya watu katika pembe mbalimbali za duniani. Vilevile utekelezaji unaotarajiwa kuanza mwaka huu wa uamuzi wa Waingereza wa kujiondoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya umezidisha wasiwasi kuhusu masuala ya kiuchumi na kifedha. Zaidi ni kwamba, iwapo mirengo ya kisiasa yenye mitazamo sawa na ile ya waungaji mkono wa Brexit (waungaji mkono wa hatua ya kuijiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya) itashinda uchaguzi wa mwaka huu nchini Ufaransa, basi kuna uwezo mkubwa kwamba mwaka 2017 unaweza kuwa mwaka wa mgawanyiko na kusambaratika Umoja wa Ulaya. 
Image Caption
Tukiachilia mbali wasiwasi uliopo kuhusu hitilafu kubwa za kisiasa na migogoro ya kiuchumi na kiusalama inayoikabili dunia katika mwaka huu wa 2017, kupasishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika siku ya mwisho ya mwaka 2016 linalounga mkono usitishaji vita nchini Syria ni hatua inayotia matumaini ambayo imeonesha kuwa, migogoro mikubwa inaweza kutatuliwa kwa njia ya ushirikiano.wa kimataifa. Mgogoro huo ulianza kutokana na uingiliaji wa madola magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu katika masuala ya ndani ya Syria na uungaji mkono wa nchi hizo kwa makundi ya kigaidi. Miongoni mwa changamoto kubwa zaidi za sasa duniani ni jinsi ya kurejesha amani na utulivu. Changamoto nyingine ni jinsi ya kulinda matunda ya azimio la aina yake la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limepiga marufuku ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina. 
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Kwa vyovyote vile, japokuwa mwaka huu wa 2017 umeanza kwa shambulizi la kigaidi la Istanbul, lakini iwapo jamii ya kimataifa itakuwa na irada na azma kubwa ya kukabiliana na vyanzo na sababu kuu za ugaidi, machafuko na migogoro wa kisiasa na kiuchumi, basi yumkini katika mwaka huu huu wa 2017 dunia ikashuhudia mabadili mengi chanya na yenye matunda kwa mwanadamu.

No comments:

Post a Comment