Baada ya kuongezeka hisia za chuki na uadui
dhidi ya Waislamu huko Amerika Kaskazini hususan baada ya kuingia
madarakani Rais Donald Trump nchini Marekani, hivi sasa matokeo mabaya
ya jambo hilo yameanza kuonekana.
Jana Jumatatu, maafisa wa Canada
walitangaza habari ya kushambuliwa msikiti mmoja na kuuliwa Waislamu
watano huko Quebec na kujeruhiwa wengine kadhaa. Waislamu 40 walikuwemo
msikitini humo wakati watu watatu wenye chuki za kidini
walipowashambulia kwa risasi. Polisi wa Quebec wamesema. watu wawili
kati ya watatu walioushambulia kwa risasi msikiti huo, wametiwa mbaroni.
Tukio hilo linaonesha ni kiasi gani
propaganda mbaya dhidi ya Waislamu zilivyo na madhara kiasi kwamba
zinaweza kusababisha mauaji ya Waislamu. Hivi sasa propaganda za chuki
dhidi ya Waislamu zimeshika kasi zaidi nchini Marekani, lakini madhara
ya propaganda hizo chafu yanaonekana hadi nje ya mipaka ya Marekani.
Ikumbukwe kuwa propaganda za chuki dhidi ya Waislamu nchini Canada ni
ndogo ikilinganishwa na Marekani. Kabla ya hapo pia msikiti wa Ranchview
katika mji wa Calgary wa jimbo la Alberta huko Canada ulishambuliwa na
watu wenye chuki za kidini. Shambulio la jana Jumatatu dhidi ya Waislamu
wa Canada limefanyika katika hali ambayo wiki za hivi karibuni,
misikiti ya nchi hiyo ilifungua milango yake kwa ajili ya kuwahudumia
watu wasio na makazi nchini humo.
Nukta ya kuzingatiwa hapa ni namna shambulio hilo lilivyosadifiana
kwa kiasi fulani na amri iliyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump ya
kuwazuia raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia Marekani. Hatua hiyo ya
serikali ya Marekani inakinzana kikamilifu na sehria za kimataifa. Hatua
hiyo imelalamikiwa vikali kote ulimwenguni. Waendesha Mashtaka Wakuu wa
majimbo 16 ya Marekani yakiwemo ya California, New York na Pennsylvania
walitoa tamko siku ya Jumapili na kulaani amri ya Trump ya kuwapiga
marufuku raia wa nchi hizo za Kiislamu kuingia Marekani.
Vitendo vya chuki na uadui dhidi ya
Waislamu vimeongezeka sana huko Amerika Kaskazini tangu baada ya kutokea
shambulio la kigaidi katika mji wa San Bernardino wa jimbo la
California huko Marekani mwezi Disemba 2015. Vile vile mahambulizi ya
kigaidi yaliyotokea hivi karibuni barani Ulaya yamezidi kuwapa
kisingizio maadui wa Uislamu kuwasakama Waislamu na kudhihirisha
waziwazi chuki zao dhidi ya wafuasi wa dini hiyo tukufu ya Mwenyezi
Mungu. Wakati wa kampeni za uchaguzi nchini Marekani, Trump alitangaza
kuwa atapiga marufuku kuingia Waislamu nchini humo kama njia ya
kukabiliana na ugaidi. Matamshi hayo ya chuki yalilaaniwa vikali katika
pembe mbalimbali za dunia, ndani na nje ya Marekani. Hata hivyo, rais
huyo mwenye chuki za kidini hakujali malalamiko hayo makubwa ya
walimwengu na ametoa amri ya kuzuia kijeuri na kinyama raia wa nchi saba
za Waislamu kuingia nchini humo.
Hivi sasa kumejitokeza wasiwasi mkubwa
wa kuongezeka vitendo vya kikatili na vya chuki za kidini dhidi ya
Waislamu wasio na hatia. Shambulio la kikatili lililofanywa dhidi ya
Waislamu tena nchini Canada ambako hakuna historia ya mashambulizi
makali kama hayo dhidi ya Waislamu linaonesha kuwa wingu jeusi la chuki
na uadui wa kidini dhidi ya Waislamu limezidi kutanda huko Amerika
Kaskazini. Hali hiyo mbaya si tu ni hatari kubwa kwa usalama wa kikazi
na kimakazi wa Waislamu wa nchini Marekani na Canada, lakini pia
Waislamu wa nchi hizo hivi sasa wana hofu ya kupoteza roho zao hata
wanapotembea mitaani na wanapokuwa kwenye nyumba zao za ibada, licha ya
mapenzi makubwa wanayowaonesha wafuasi wa dini nyinginezo na
kuwathibitishia kuwa propaganda zote dhidi yao zinatokana tu na chuki za
kidini za maadui wa Uislamu.
No comments:
Post a Comment