Thursday, January 26, 2017

POLISI NIGERIA WAWAFYATULIA MABOMU YA KUTOWA MACHOZI WAFUASI WA SHEIKH ZAKZAKY

Maafisa usalama nchini Nigeria wamewafyatulia mabomu ya kutoa machozi wafuasi wa kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye anaendelea kuzuiliwa kinyume cha sheria.
Shirika la habari la Press TV limeripoti kuwa, mamia ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky hapo jana walifyatuliwa mabomu ya kutoa machozi walipokuwa wakishiriki maandamano ya amani ya kuonyesha uungaji mkono wao kwa kiongozi wao, nje ya bunge la nchi hiyo katika mji mkuu Abuja.
Maafisa wa polisi wa Nigeria waliyavunja maandamano hayo ya amani kwa mabomu ya machozi, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa. Waandamanaji hao ambao walikuwa wamebeba picha za Zakzaky na maberamu yenye ujumbe unaosema, "Muachieni huru Zakzaky" walisikika wakiikosoa vikali serikali ya Abuja kwa kuendelea kumzuilia Sheikh Zakzaky licha ya agizo la mahakama.
Maandamano ya amani Abuja ya kushinikiza kuachiwa huru Sheikh Zakzaky
Itakumbukwa kuwa Mahakama ya Shirikisho la Nigeria hivi karibuni ilitoa amri ya kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, lakini serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo inavunja waziwazi amri hiyo ya mahakama kwa kukataa kumwachilia huru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu.
Umoja wa Ulaya na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International ni baadhi ya taasisi za kimataifa zilizotoa taarifa zikiwataka viongozi wa Nigeria kuheshimu amri ya mahakama ya kumwachilia huru mara moja kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment