Tuesday, January 10, 2017

KIFO CHA RAFSANJANI; MSAIDIZI MKONGWE WA IMAMU NA KIONGOZI WA MAPINDUZI YA KIISLAMU, KATIKA MTAZAMO WA VYOMBO VYA HABARI VYA KIGENI

Tokea aage dunia Hashimi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran hapo siku ya Jumapili jioni, vyombo vya habari na duru nyingi za kisiasa za kimataifa zimekuwa zikichambua kwa kina historia na maisha ya shakhsia huyo muhimu.
Bila shaka jambo hilo linabainisha wazi nafasi muhimu na maalumu aliyokuwa nayo Hashimi Rafsanjai katika mfumo mzima wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kwamba kuaga kwake dunia bila shaka ni msiba mkubwa kwa mfumo huu. Vyombo hivyo vya habari ikiwemo BBC ambayo ilikatiza ratiba zake za kawaida za utangazaji na kurusha hewani vipindi maalumu vya historia ya Mapinduzi ya Kiislamu na maisha pamoja na nafasi ya Hashimi Rafsanjani katika mapinduzi hayo, vilidai kwamba mazishi ya Rafsanjani yanaweza kuchambuliwa katika mitazamo miwili, mmoja ukiwa ni kwamba mazishi yake ni ya kiserekali na wa pili ni kwamba ni fursa kwa wale wasioridhishwa na hali ya mambo au wanaounga mkono misimamo na mitazamo yake, hasa mwishoni mwa umri wake, kudhihirisha matakwa yao hadharani. Muelekeo huo wa kihabari ambao umekuwa ukifuatiliwa na vyombo vingi vya habari vya magharibi unataka kuthibitisha kwamba kumekuwepo na hitilafu za mitazamo kati ya marehemu Rafsanjani na viongozi wengine wa Mfumo wa Kiislamu.
Swala ya maiti ya Rafsanjani ikiongozwa na Ayatullah Ali Khamenei
Pamoja na hayo hata tukifaradhisha kuwepo kwa hitilafu na tofauti kama hizo za kimtazamo kuhusiana na baadhi ya sera za kisiasa za Rafsanjani, kwa hakika jambo hilo halipaswi kupingwa wala kuchukuliwa kuwa baya, bali hiyo ni moja ya nukta muhimu na chanya katika muundo wa Mfumo wa Mapinduzi ya Kiislamu, nukta ambayo inathibitisha wazi uwezo na uvumilivu mkubwa uliopo miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa mfumo huu. Hakuna shaka yoyote kwamba Hashimi Rafsanjani katika hilo ameweza kudhihirisha mfano bora na kuthibitisha kwa maneno na vitendo kwamba licha ya kuwa na mitazamo tofauti na huru kuhusiana na baadhi ya mambo lakini wakati huohuo inawezekana kusalia kwenye misingi na hivyo kulinda umoja wa kitaifa na kuifanya sheria kuwa kigezo kinachopasa kufuatwa na kuzingatiwa na wote katika uchukuzi wa maamuzi. Alithibitisha wazi suala hilo wakati alipoamua kutii sheria na kutovuka mistari myekundu ya sheria kwa kuafikiana na uamuzi wa mahakama wakati mtoto wake mwenyewe alipohukumiwa kwenda jela kutokana na baadhi ya masuala ya kisheria.
Rafsanjani katika kipindi cha vita vya kulazimishwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu
Kwa msingi huo tunapasa kusema kuwa hitilafu za mitazamo ni jambo linalopasa kuwepo katika kila jamii yenye harakati na uhai  la sivyo jamii hiyo hupoteza uhai huo. Sula muhimu hapa ni jinsi ya kulitazama jambo hilo. Hii ni nukta ambayo Rafsanjani mwenyewe amekuwa akiisisitiza mara kwa mara na hasa baada ya matukio ya fitna ya 2009 ambapo licha ya kuwa na msimamo tofauti kuhusiana na matukio hayo lakini alisisitiza sana kulindwa thamani za Mfumo wa Kiislamu na kufuatwa amri za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa mtazamo huo Ayatullah Hashimi Rafsanjani alilichukulia suala la umoja kuwa nguzo muhimu ya kulindwa mfumo huu na kigezo cha kutathminiwa tabia na misimamo ya kisiasa katika vipindi muhimu vya Mapinduzi ya Kiislamu. Alikuwa akiamini kwa dhati kwamba Mapinduzi na Mfumo huu ni wa wananchi wote na kwamba mirengo yote ya kisiasa na kifikra nchini inapata uhalali wao kutokana na uungaji mkono wa wananchi na kwa hivyo maslahi yao ya kitaifa hayapasi kufanywa kuwa muhanga wa maslahi ya kisiasa ya watu maalumu. Katika miaka ambayo nchi iliathirika kutokana na matokeo ya uchaguzi wa rais wa duru ya kumi, alichambua mambo mbali kabisa na hisia na ushabiki wa kisiasa na kujaribu kutuliza mivutano na kuielekeza kwenye mkondo wa sheria. Hata kama alikuwa na mitazamo na matatizo fulani kuhusiana na hali iliyojitokeza nchini katika kipindi hicho lakini alikuwa akiyawasilisha na kuyazungumzia katika ngazi za juu za mfumo na sio kuropokwa ovyo ili kulinda umoja na mshikamano wa kitaifa.
Halaiki ya wananchi katika mazishi ya Hashimi Rafsanjani
Katika upande wa pili vyombo vya habari vya kigeni ambavyo havijasita kufanya njama za kuonyesha kuwepo mgawanyiko mkubwa miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa Mfumo wa Kiislamu mara hii pia vimejaribu kutumia fursa ya kifo cha Hashimi Rafsanjani kujaribu tena kusisitiza suala la kuwepo hitilafu kubwa kati ya marehemu na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Mfumo wa Kiislamu. Hii ni katika hali ambayo Rafsanjani mwenyewe katika utekelezaji wa majukumu yake ya kimapinduzi alikuwa akiuzingatia sana mustakbali wa Mfumo wa Kiislamu na nchi nzima kwa ujumla na hasa kuhusiana na suala zima la uongozi wa masuala ya kiuchumi na kisiasa ili kuimarisha nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu. Akiwa mwanamapinduzi halisi na shakhsia muhimu na mwenye busara wa kisiasa nchini, Ayatullah Rafsanjani aliweza kutekeleza ipaswavyo na kivitendo majukumu aliyokuwanayo na hivyo kutoa mchango mkubwa katika kulinda Mapinduzi ya Kiislamu na kukabidhi thamani zake kwa vizazi vijavyo vya mapinduzi hayo.

No comments:

Post a Comment