Monday, January 2, 2017

WATU 36 WAUAWA KATIKA HUJUMA YA KIGAIDI MJINI BAGHADAD

Watu wasiopungua 36 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa leo kufuatia hujuma ya kigaidi katika kitongoji cha Sadr katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.
Duru za usalama Iraq zinasema hujuma hiyo ilitokea katika kituo cha mabasi katika kitongoji cha Sadr ambacho wakaazi wake wengi  ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh limetoa taarifa na kudai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi ambayo imewalenga raia wasio na hatia.
Kwingineko magaidi wa ISIS wameshambulia kwa kombora katika mtaa wa Al Tamim mashariki mwa mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq kuwaua raia 18.
Wananchi wakikusanyika eneo la milipuko katika kitongoji cha Sadr mjini Baghdad
Huku hayo yakijiri, vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Iraq vimetoa taarifa na kusema vimefanikiwa kuzuia hujuma za magaidi katika mikoa ya Najaf al Ashran na Karbala.
Imedokezwa kuwa magaidi hao walikusudia kuingia katika mikoa hiyo miwili kwa kupitia eneo la An Nakhib ambapo kulijiri mapigano baina ya magaidi na vikosi vya kujitolea vya wananchi na kupelekea magaidi sita kuuawa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, viongozi wa Iraq wameendelea kusisitiza azma ya serikali ya nchi hiyo ya kupambana na makundi ya kigaidi kwa hali na mali hadi itakapong'oa mizizi ya magaidi yao katika ardhi ya nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment