Thursday, January 26, 2017

RAIS BARROW AREJEA GAMBIA, ATAKA KIKAO CHA KIENEO KIBAKIE NCHINI MIEZI 6

Rais mpya wa Gambia Adama Barrow amerejea nchini kwake leo Alkhamisi akitokea nchi jirani ya Senegal, ambayo alilazimika kuigeuza kimbilio lake tangu Januari 15, akihofia usalama wake.
Mohammed Ibn Chambas, afisa wa Umoja wa Mataifa katika eneo la magharibi mwa Afrika amewaambia waandishi wa habari nchini Senegal kuwa, Barrow ameomba kikosi cha askari wa kieneo kisalie nchini humo kwa miezi sita zaidi, hadi mambo yatakapotengamaa. Afisa huyo wa UN ameongeza kuwa, uamuzi wa mwisho wa ombi la Rais Barrow utatolewa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS.
Rais Barrow akiapishwa katika ubalozi wa Gambia nchini Senegal wiki jana
Msemaji wa Barrow, Halifa Sallah amethibitisha kuwa, rais huyo mpya wa Senegal anaingia nchini leo na kwamba sherehe za kumpokea zitafanyika baadaye.
Rais Barrow anarejea Gambia baada ya kuondoka mtangulizi wake aliyeiongoza nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika kwa miaka 22, Yahya Jammeh.
Jammeh ambaye yuko uhamishoni nchini Equatorial Guinea, anadaiwa kuondoka nchini Gambia na dola milioni 11 za Marekani kutoka hazina ya taifa, tuhuma ambazo kiongozi mpya wa taifa ameagiza zichunguzwe.
Yahya Jammeh akiondoka Banjul, Gambia
Wananchi wa Gambia wana matarajio mengi kutoka kwa uongozi wa Barrow. Tayari rais huyo mpya wa Gambia amemteua afisa wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Fatoumata Tambajang kuwa makamu wake.

No comments:

Post a Comment