Sunday, January 1, 2017

IRAN YAKANUSHA KUPOKEA BARUA YA SAUDIA YA MWALIKO WA HIJA

Mkuu wa Shirika la Hija na Ziara la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekanusha madai ya Saudi Arabia kuwa imetuma barua ya mwaliko kwa Iran wa kushiriki kwenye Hija ya mwaka ujao.
Siku ya Alkhamisi iliyopita, Waziri wa Hija na Umra wa Saudi Arabia, Muhammad Benten alitangaza kuwa Riyadh imetoa mwaliko kwa ujumbe wa Shirika la Hija na Ziara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuhudhuria kikao cha kuratibu maandalizi ya Hija.
Hamid Muhammadi, Mkuu wa Shirika linaloshughulikia masuala ya Hija na Ziara la Iran amevieleza vyombo vya habari kuwa hakuna barua ya mwaliko iliyotumwa na Saudia kwa ajili ya Hija ya mwaka ujao na kusisitiza kwamba Shirika la Hija na Ziara na Ofisi ya Kiongozi Muadhamu ya Masuala ya Hija zinafuatilia kwa uwezo wao wote kuondolewa vizuizi vya Hija.
Muhammadi ameongeza kuwa kuvunjwa uhusiano wa kisiasa kati ya Iran na Saudia kumesababisha kufungwa ubalozi wa Iran mjini Riyadh na balozi zake ndogo zilizoko mjini Jeddah na kwamba ikiwa serikali ya Saudi Arabia itatekeleza masharti yanayodhamini izza, usalama na heshima ya mahujaji na wafanya ziara wa Iran, Jamhuri ya Kiislamu itashiriki katika Hija ijayo.
Maafa ya Mina
Itakumbukwa kuwa kutokana na usimamizi mbovu wa utawala wa Aal Saud katika Hija ya mwaka jana, zaidi ya mahujaji elfu saba wakiwemo mahujaji 477 kutoka Iran walifariki dunia katika maafa mawili yaliyotokea kwenye msikiti mtukufu wa Makka na eneo la Mina.
Kwa kutumia kisingizio cha madai yasiyo na msingi, serikali ya Saudia mwaka huu iliwazuilia njia ya kutekeleza ibada tukufu ya Hija wafanya ziara wa baadhi ya nchi za Kiislamu ikiwemo Iran na Syria…/

No comments:

Post a Comment