Monday, January 30, 2017

CHINA: TAHADHARI YA KUTOKEA VITA NA MAREKANI SIO MANENO TU BALI NI KWELI HALISI

Viongozi wa China wamesema kuwa, indhari ya kutokea vita kati ya nchi hiyo na Marekani katika kipindi cha Rais Donald Trump, sio madai pekee, bali ni ukweli halisi.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika jeshi la China ambaye hakutaka kutaja jina lake sambamba na kusema maneno hayo ameongeza kuwa, katika kujiandaa na vita na Marekani, jeshi la nchi hiyo limeweka mfumo wa ulinzi wa makombora katika bahari ya kusini na mashariki mwa China, kwa ajili ya ulinzi wa Peninsula ya Korea. Afisa huyo wa jeshi la China amesisitiza kuwa, Beijing imeingia katika awamu mpya ya kujiimarisha kiulinzi kutokana na hatari inayolikabili eneo la kusini mashariki mwa Asia.
Jeshi la Uchina
China imechukua hatua hizo kutokana na matamshi ya uhasama ya rais mpya wa Marekani Donald Trump dhidi ya nchi hiyo. Hivi karibuni pia jeshi la China lilitangaza kuwa, kuendelea kuwa mbaya hali ya mambo kuhusiana na usalama wa bahari ya eneo, machafuko katika eneo la Asia na Bahari ya Pasifiki na kadhalika misimamo tata ya rais huyo mpya wa Marekani, inailazimu kujiandaa kuingia katika vita tarajiwa na Marekani kuliko wakati mwingine wowote ule.
Jeshi la Uchina likiwa katika maandalizi
Ripoti hiyo ya jeshi la China ilifafanua kuwa, msimamo wa Washington wa kuweka ngao ya makombora ya THAD nchini Korea Kusini, kuongeza idadi ya askari wake katika maeneo ya mashariki na kusini mwa bahari za Uchina na kadhalika kuanzisha mlingano mpya wa kijeshi barani Asia, ni siasa ambazo zinaweza kuwasha moto wa vita wakati wowote. Mwezi Disemba mwaka jana, Donald Trump alitangaza kuwa, Washington haitafungamana na siasa za 'China Moja' kuhusiana na uhusiano wa nchi yake na Taiwan, suala ambalo lililalamikiwa na Beijing.
Makomando wa jeshi la China wakiwa katika mafunzo
Hii ni kwa kuwa mara kadhaa Beijing imekuwa ikitangaza kuwa, siasa za 'China Moja' ni suala lisilo na mjadala huku ikiitaka Washington kuangalia upya siasa zake kuhusiana na suala hilo.

No comments:

Post a Comment