Tuesday, January 17, 2017

IRAN ITAKABILIANA NA HATUA ZA MAREKANI ZA KUTAKA KUVURUGA MAPATANO YA NYUKLIA

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Iran itakabiliana na hatua ya Marekani ya kukiuka majukumu yake katika utekelezaji wa mapatano ya nyuklia yajulikanayo kwa jina la "Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA)."
Rais Rouhani ameyasema hayo leo alasiri mjini Tehran katika kikao cha kimataifa cha waandishi habari kwa mnasaba wa kutumia mwaka moja tangu kuanza kutekelezwa mapatano ya JCPOA.
Rais Rouhani ameashiria hatua ya Marekani ya kuvunja ahadi na kuvuruga utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia na kuongeza kuwa: "Serikali na taifa la Iran litakabiliana kwa nguvu na uvunjaji ahadi huo na wala halitalegeza msimamo kuhusu maslahi ya taifa."
Huku akiashiria mafanikio ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na nchi za kundi la 5+1 ambazo ni China, Russia, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani, amesema: "JCPOA ni mafanikio makubwa kwa taifa la Iran."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria suala la kuondolewa Iran katika kipengee cha saba cha hati ya Umoja wa Mataifa na kusema: "Urutubishaji madini ya urani ni haki ya taifa la Iran, na Umoja wa Mataifa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umetambua rasmi shughuli za nyuklia za Iran kwa malengo ya amani."
Rais Rohani akihutubia waandishi habari mjini Tehran, Jan.17.2017
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vyote vya nyuklia dhidi ya Iran viliondolewa baada ya kuanza kutekelezwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyotiwa saini Julai mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa Januari mwaka jana.
Rais Rouhani amesema Iran ni nchi yenye taathiri katika eneo la Mashariki ya Kati na dunia na kuongeza kuwa: "Katika masuala mbalimbali ya dunia, Iran ni nchi yenye nafasi muhimu na kutokuwepo Iran katika masuala ya kisiasa ya kieneo ni hasara kwa dunia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema chuki dhidi ya Iran (Iranophobia) ni mbinu isiyo sahihi na kuongeza kuwa, Iran inataka amani na usalama katika eneo hili na dunia nzima.

No comments:

Post a Comment