Mgogoro mwingine wa kidiplomasia kati ya Kenya na Uganda unanukia. Hii ni baada ya makumi ya wahamiaji haramu raia wa Uganda kukamatwa na maafisa wa polisi wa Kenya katika mpaka wa nchi mbili hizo.
Wambua Katiithi, Kamanda Mkuu wa Polisi katika mji wa Bumula, kaunti ya Busia amesema wahajiri haramu 53 wa Uganda wamekatwa wakiwa hawana vyeti vinavyohitajika vya usafiri, wakiwa njiani kuelekea mjini Nairobi kwa kutumia usafiri wa basi.
Tukio hilo lilifanyika hapo jana, ikiwa ni chini ya masaa 24 baada ya polisi ya Uganda kuwatia mbaroni askari polisi watatu wa Kenya na wavuvi kadhaa kati ya visiwa vya Mageta na Hama katika Ziwa Victoria.
Kenya na Uganda zimekuwa zikivutana kwa miaka kadhaa sasa kuhusu masuala kadha wa kadha na haswa umiliki wa kisiwa cha Migingo, kilichoko katika mpaka wa nchi mbili hizo za Afrika Mashariki.
Mwaka jana, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema kisiwa cha Migingo katika Ziwa Victoria ni milki ya Kenya.
Mgogoro wa kisiwa cha Migingo ulianza mwaka 2008 baada ya wanajeshi wa Uganda kukivamia na kuwatimua Wakenya ingawa kimekuwa kikitambuliwa kuwa ni milki ya Kenya.
Makubaliano ya awali kati ya Kenya na Uganda kuhusu kisiwa hiki yalifanyika 2016, na kwa sasa maafisa wa usalama kutoka nchi zote mbili wanalinda doria katika kisiwa hicho.
Rais wa Marekani Donald Trump na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un wamekubaliana kuondoa kabisa silaha za kinyuklia katika rasi ya Korea katika makubaliano ya pamoja ya kihistoria.
Viongozi hao walikamilisha siku ya kihistoria ambayo ilishuhudia viongozi hao wawili wakikutana kwa mara ya kwanza kabisa.
Katika mkutano huo Trump ameahidi kuipatia Korea kaskazini uhakikisho wa usalama wake pamoja na kutangaza katika mkutano na waandishi habari baadaye kwamba Marekani na Korea kusini zitaacha luteka ya pamoja ya kijeshi kama Korea kaskazini inavyodai.
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un (kushoto) na rais wa Marekani Donald Trump wakipeana mikoni
Katika waraka wenye vipengee vinne, Marekani na Korea kaskazini zimeazimia kuweka uhusiano mpya kati ya nchi hizo mbili, kujenga utawala imara na endelevu kuelekea amani akisisitiza azimio la Panmunjeom kutoka Aprili 27.
Katika mkutano na waandishi habari leo rais Donald Trump wa Marekani amesema kwamba jeshi la Marekani litaacha kufanya mazowezi ya pamoja na Korea kusini yakiilenga Korea kaskazini, akisema yanaongeza hali ya wasi wasi na kuyasitisha kutasaidia kuhifadhi fedha nyingi zinazotumika katika mazowezi hayo. Pia amesema atamwalika kiongozi wa Korea kaskazini katika ikulu ya marekani White house na kwamba binafsi angependa kutembelea mji mkuu wa Korea kaskazini Pyongyang.
Nchi hizo mbili hufanya mazowezi ya kijeshi kila mwaka ambayo yanaikera Korea kaskazini , ambayo imekuwa kwa muda mrefu ikidai kusitishwa kwa mazowezi hayo na mara nyingi hujibu kwa kuchukua hatua zake, na kusababisha kuongezeka kwa hali ya wasi wasi.
Rais Trump akionesha waraka uliotiwa saini baina yake na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un
Kim amshukuru Trump
Wakati wa kutia saini makubaliano hayo kati ya Trump na Kim leo asubuhi, rais Trump alisema pande zote mbili zimefurahi kutia saini makubaliano hayo.
"Tunatia saini waraka muhimu sana, waraka ambao una maelezo mapana. na tutajadili hili kwa kina. Kwa hivi sasa naamini mtapata nakala kwa niaba ya mwenyekiti Kim na mimi. Na wote tunafahari kubwa kutia saini waraka huu. Asante."
Kwa upande wake kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un alimshukuru rais Trump kwa kukubali kufanyika mkutano huo.
"Leo tulikuwa na mkutano wa kihistoria na kuamua kuacha nyuma yaliyopita. Na tuko tayari kutia saini waraka huu wa kihistoria. Dunia itaona mabadiliko makubwa. Napenda kueleza shukurani zangu kwa rais Trump kwa kufanikisha mkutano huu. Asante.
Kuhusu vikwazo dhidi ya Korea kaskazini rais Trump amesema kwa hivi sasa vikwazo hivyo vitaendelea , lakini anaangalia uwezekano wa kuviondoa.
Rais Trump akiwa katika mkutano na waandishi habari baada ya kutia saini makubaliano na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un
Rais wa Marekani amesema pia kwamba kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un ana nia thabiti ya kuharibu kabisa maeneo ambayo nchi hiyo inafanyia majaribio silaha zake.
Kwa upande mwingine waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na mwenzake wa Malaysia mahathir Mohammed wamekubaliana leo kufanyakazi kwa pamoja kupambana na mipango ya kinyuklia na makombora ya Korea kaskazini. Viongozi hao wamesema wanataka kutuma ujumbe mkali kwa Korea kaskazini kuhusu suala hilo. Waliysema hayo katika mkutano na waandishi habari kufuatia mkutano wao mjini Tokyo
Magazeti ya Ujerumani yamemtaja Rais Donald Trump wa Marekani kuwa ni mtu asiyejua mipaka yake wala asiye na mantiki na yamezitaka nchi zote za Ulaya kuacha kumfuata kiongozi huyo.
Gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung limeripoti kuwa, kila mtu aliyekuwa anaamini kuwa Rais wa Marekani ni mtu mwenye mantiki na anayetilia maanani uhakika wa mambo anapaswa kuzika matumaini hayo kwa sababu kuwepo kwa mtu huyo asiye na adabu na mbumbavu hakuifanyi dunia kuwa sehemu bora na yenye amani zaidi.
Gazeti hilo la Ujerumani limeongeza kuwa: Trump anaendelea kuzitishia nchi nyingine kwa kutumia mabavu na silaha ya uchumi, na suala hilo ni hatari sana kwa Ujerumani.
Süddeutsche Zeitung limeandika kuwa: Nchi za Magharibi zimekumbwa na mgawanyiko katika masuala ya kisiasa na uhakika huo umeonekana waziwazi katika mkutano wa viongozi wa nchi 7 zilizopiga hatua kiviwanda wa G7 huko Canada ambao kimsingi ulibadilika na kuwa G6.
Rais Donald Trump wa Marekani siku chache zilizopita aliwaacha bumbuazi viongozi wengine wa G7 katika mkutano wa Canada baada ya kuondoka ghafla katika mkutano huo na kufuta saini yake katika hati ya mwisho ya mkutano huo.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amebainisha masiktiko yake baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kukataa kuidhinisha taarifa ya mwisho ya kikao cha viongozi wa nchi tajiri kiviwanda G7 ambacho kilimalizika juzi huko Quebec, nchini Canada. Merkel amebainisha wazi kuwa nchi za Ulaya hazipaswi kuitegemea tena Marekani.
Naye Heiko Maas Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesisitiza kuwa, jibu la Ulaya kuhusu uamuzi huo wa Trump linapaswa kuwa ni mshikamano na ukuruba zaidi katika Umoja wa Ulaya.
Mass ameongeza kuwa uamuzi wa Trump wa kutoafiki taarifa ya mwisho ya kikao cha G7 haukuzishangaza sana nchi shiriki kwani Trump amekiuka mapatano mengine muhimu ya utunzaji mazingira na mapatano ya nyuklia ya Iran.
Baada ya mkutano wa viongozi wa kundi la G7, kumedhihirika hitilafu kubwa na za wazi baina ya Rais Trump na viongozi wa Canada, Ufaransa na Ujerumani. Trump aliondoka mapema kabla ya kikao hicho kumalizika kama ishara ya kubainisha kuchukizwa kwake na tamko la Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na kusema hataunga mkono taarifa ya mwisho ya kikao hicho. Uamuzi huo wa Trump umetajwa kuwa ni pigo kubwa kwa kundi la G7 ambalo linajumuisha Marekani, Canada, Ujerumani, Uingereza,Ufaransa, Italia na Japan.
Hatua hiyo ya Trump itatoa pigo kubwa kwa ushirikiano wa pande mbili za Bahari ya Atlantiki na pia ni pigo kubwa kwa uhusiano wa kistratijia wa Canadan na Marekani. Kwa hatua yake hiyo, Trump analenga kung'oa mizizi ya uhusiano na mshikamano wa miongo kadhaa wa kiuchumi, kibiashara, na kiusalama baina ya Marekani na Ulaya. Wakuu wa Ulaya wanajaribu kuzuia hali ya mambo kuwa mbaya zaidi na wanasema hatua ya Trump kutosaini taarifa ya mwisho haimaanishi kila kitu kimekwisha. Kuhusiana na hili, Angela Merkel amesema: "Hatua ya Trump kutangaza kuwa hatatia saini taarifa ya mwisho ya G7 kupitia Twitter ni jambo la kusikitisha. Ameongeza kuwa, 'kikao cha viongozi wa G7 huko Canada hakikuwa mwisho wa ushirikiano wa Ulaya na Marekani lakini akaongeza kuwa, nchi za Ulaya hazipaswi kuitegemea tena Marekani na zinapaswa zenyewe zijiamulie hatima yao.'
Ingawa suala la Marekani kujiondoa G7 halijapewa uzito mkubwa lakini kwa kuzingatia utendaji kazi wa Trump katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu wa urais wake, nchi zingine sita za kundi la G7 hazitashangaa iwapo Trump ataendeleza mwenendo wake huo wa kupuuza na kubatilisha mikataba ya kimataifa, na hivyo aamue kujiondoa katika kundi hilo. Kwa hivyo nchi hizo sita zinajitayarisha kwa hali kama hiyo.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anasema hivi kuhusu suala hilo:"Pengine Trump hajali iwapo atatengwa lakini hata tukibadilika na kuwa kundi la G6 bado tutakuwa nguvu kubwa. Iwapo Trump ataamua kuiondoa Marekani katika nafasi yake duniani, jambo hilo litakuwa na matokeo hasi kwa uchumi na hadhi ya Marekani duniani. Trump anafahamu hili."
Mtazamo wa Trump kuhusu masuala ambayo yamepelekea kuibuka hitilafu baina ya Marekani na Ulaya ni jimbo linaloonyesha kuwa hana nia ya kulegeza msimamo wake bali hata ametoa vitisho kwa kwa nchi za Ulaya na Canada hasa katika masuala ya kibiashara. Trump ameongeza kwa kiwango kikubwa ushuru wa bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka Ulaya, Canada na Mexico hasa bidhaa za chuma.
Hatua hizo za Trump zimepelekea kuongezeka hitilafu kubwa baina ya Marekani na nchi hizo na kuwepo hatari ya kuibuka vita vya kibiashara kati ya Marekani na nchi hizo. Hali kadhalika nchi za Ulaya pia zimekasirishwa na hatua ya Trump ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA na mapatano mengine muhimu ya mazingira maarufu kama Mapatano ya Tabianchi ya Paris.
Kwa mtazamo wa nchi muhimu katika Umoja wa Ulaya, si tu kuwa sera za Trump zitaidhuru dunia bali zitapelekea kutengwa zaidi Marekani katika uga wa kimataifa.
Watu 30 wameuawa katika mapigano kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wanamgambo wa Mai-Mai mashariki mwa nchi hiyo.
Duru za eneo hilo zimeripoti kuwa katika mapigano hayo yaliyotokea jana na kuendelea kwa saa kadhaa wanajeshi 18 waliuawa akiwemo afisa mmoja na kamanda wa polisi wa polisi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa duru hizo, wanamgambo wanane waliohusika katika hujuma hiyo pamoja na raia watatu pia waliuawa katika mapigano hayo. Raia hao waliuliwa kwa risasi walipokuwa wakikimbia mapigano.
Mnamo siku ya Alkhamisi iliyopita, wanamgambo wa kundi la Mai-Mai walilidhibiti eneo lenye utajiri wa madini la Salamambila mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini wakalazimika kuliacha na kukimbia baada ya vikosi vya jeshi la serikali kufika katika eneo hilo.
Wanamgambo wa Mai-Mai wanatokana na makundi ya wabeba silaha waliopata mafunzo ya kijeshi katika eneo la mashariki mwa Kongo DR ambalo limekuwa uwanja wa mapigano kwa zaidi ya miaka 20 sasa.../
Rais Hassan Rouhani amesema, baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya JCPOA waliowengi katika jamii ya kimataifa wameipa haki Iran na kuyatetea makubaliano hayo na kuongeza kwamba hatua zilizochukuliwa hadi sasa ni nzuri kwa ajili ya kuendeleza makubaliano hayo ya nyuklia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyaeleza hayo mbele ya hadhara ya maulamaa na wanazuoni wa mjini Tehran na kubainisha kuwa: Leo akthari ya nchi zinaitakidi kuwa njia iliyofuata Iran ilikuwa sahihi na Marekani ndio iliyofanya makosa, na hayo ni mafanikio makubwa.
Rais Rouhani amefafanua kuwa Marekani inatoa mashinikizo kwa nchi za Ulaya kwamba zichague kati ya Marekani na Iran lakini nchi hizo zinasema 'sisi tunachagua makubaliano ya JCPOA'.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa msingi inaofungamana nao Iran ni kwamba kama itaweza kupata haki zake kwa kubaki kwenye makubaliano ya JCPOA itaendelea kufungamana na makubaliano hayo ya kimataifa.
Ikumbukwe kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza Mei 8 kuwa nchi yake imejiondoa katika mapatano hayo ya nyuklia ya Iran ambayo rasmi yanajulikana kama JCPOA. Trump aidha alisema ataiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vya nyuklia katika kipindi cha miezi mitatu hadi sita ijayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa mno na uamuzi huo wa upande mmoja uliochukuliwa na rais wa Marekani.
Hii ni katika hali ambayo nchi zilizosalia katika JCPOA, yaani Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Ujerumani na Umoja wa Ulaya, zimesisitiza kuwa zitandelea kuunga mkono mapatano hayo.
Wakati huohuo katika siku za karibuni Iran na nchi za Ulaya zimefanya mazungumzo kadhaa kwa lengo la kuyaendeleza makubaliano ya JCPOA baada ya Washington kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.
Inafaa kukumbusha pia kuwa mnamo siku ya Jumatano iliyopita Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alibainisha masharti ya Iran kuendelea kubakia katika JCPOA na kusisitiza kuwa: "Nchi za Ulaya zinapaswa kuwasilisha azimio dhidi ya Marekani katika Baraza la Usalama, ziahidi pia kuwa kadhia za makombora na ushawishi wa Iran katika eneo hazitajadiliwa na pia zikabiliane na vikwazo vyovyote vya Marekani dhidi ya Iran." Aidha Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa nchi za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kununua mafuta ya Iran kwa kiwango ambacho Iran inahitaji na pia benki za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kutekeleza malipo ya kifedha kwa ajili ya biashara na serikali pamoja na sekta binafsi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.../
Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Jasem Al-Najem anashiriki katika utekelezaji wa programu ya kufuturisha ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambayo inafadhiliwa na Chombo cha Baytu Zakat, Wakfu na Mali ya Amana ya Kuwait. Programu kama hii huandaliwa kila mwaka kutoka kwa wasamaria wa nchi ya Kuwait.
Programu hii thamani yake ni dola elfu 26 na mia nne sawa na shilingi milioni 60.
Awamu ya kwanza ya programu hii ilikuwa ni kugawa vikapu 400 vyenye vyakula kama mchele, sukari,unga,mafuta ya kula, tende na sukari ambapo katika moja ya zoezi la ugawaji alihudhuria Mkuu wa Wilaya ya Ilala. Bi Sophia Mjema.
Ubalozi wa Kuwait umedhamiria mwaka huu kuwasilisha misaada ya futari katika miji, vitongoji, kata, mitaa, vijiji na maeneo ya mbali kote Tanzania ambapo hadi sasa mikoa ya Tanga, Iringa, Dar es salaam na visiwa vya Zanzibar imefaidika na misaada hiyo ambayo Ubalozi hushirikiana na asasi zisizokuwa za kiserikali za Tanzania katika kuwafikia walengwa.
Watu wasiopungua 15 wameaga dunia huko Somaliland baada ya mvua kubwa zilizosababishwa na kimbunga cha kitropiki kwa jina la Sagar kuiathiri nchi hiyo ya Pembe ya Afrika mwishoni mwa wiki.
Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991. Abdirahman Ahmed Ali Gavana wa eneo la Awdal amesema kuwa mvua kubwa zilizonyesha katika muda wa masaa 24 yaliyopita zimeua watu 16 katika wilaya za Lughaya na Baki. Serikali ya Somaliland tayari imeanza kutoa misaada ya dharura kwa wahanga wa kimbunga hicho. Wakati huo huo upepo mkali uliosababishwa na kimbunga cha Sagar umewasomba wanaume wawili pamoja na gari yao huko katika mji wa Bosaso katika eneo la Puntland, huko kaskazini mashariki mwa Somalia. Hayo yameelezwa na Yusuf Mohamed Waeys Gavana wa Bari katika eneo la Puntland.
Wakati huo huo Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayohusika na Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu imesema kuwa maelfu ya watu wameathirika na mafuriko hayo, wamepoteza makazi na miundo mbinu kuharibiwa huko Puntland.
Watu watatu tu wameripotiwa kunusurika katika ajali ya ndege iliyochakaa aina ya Boeing 737 ambayo ilianguka hapo jana muda mfupi baada ya kuruka katika uwanja wa ndege wa Havana nchini Cuba huku wachunguzi wakijaribu kubaini chanzo cha ajali hiyo kupitia mabaki ya ndege hiyo.
Kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya Cuba hali ya hewa ilikuwa ya mawingu na mvua ilikuwa inanyesha wakati ndege hiyo ambayo imeshatumika kwa muda wa miaka 39 ilipoanguka ikiwa katika safari za ndani kuelekea mji wa Holguin mashariki mwa nchi hiyo.
Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba amesema tume maalumu imeundwa kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 104, akthari yao wakiwa ni Wacuba pamoja na wahudumu sita.
Abiria wanne walionusurika walipelekwa hospitali ya Havana, ambapo hadi kufikia jana usiku watatu miongoni mwao walikuwa wangali hai.
Ajali hiyo ya jana ya ndege imetajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Cuba katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita na ya tatu kwa ukubwa kutokea duniani tangu mwaka 2010.../
Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine ametoa matamshi mabaya yenye kuwavunjia heshima wahajiri au wahamiaji nchini humo kwa kuwataja kuwa ni wanyama.
Matamshi hayo ya Trump si ya kwanza ya aina yake kwani miezi kadhaa iliyopita katika kikao chake na wajumbe wa vyama vya Democrat na Republican katika Ikulu ya White House aliashiria kuhusu wahajiri kutoka Haiti, El Salvador na baadhi ya nchi za Afrika na kuzitaja kuwa sawa na shimo la kinyesi.
Matamshi hayo ya mara kwa mara ya Trump ya kuwavunjia heshima wahamiaji hasa wenye asili ya Afrika yamekosolewa na wajumbe wa chama cha upinzani cha Democrat ambao wanasema ni ishara ya wazi kuwa mtawala huyo ni mbaguzi wa rangi.
Ikulu ya White House ilijaribiu kuonyuesha kuwa matamshi hayo yalitokana na hisia za kitaifa za rais huyo, lakini baada ya kuendelea malalamikio kuhusu matamshi hayo ya kishenzi ya Trump, rais huyo akiwa katika mkutano na Katibu Mkuu wa Shirika la Kijeshi la Nato, katika kujaribu kutetea matusi yake kuhusu wahajiri wanaoingia nchini humo kinyume cha sheria, amesema wakati alipowahutubu kwa kuwaita kuwa ni 'Wanyama' siku ya Jumatano, alikusudia genge la wahalifu linalojulikana kama 'MS 13'.
Matamshi hayo ya Trump kuhusu wahajiri ambayo aliyatoa wakati wa mkutano wake na wakuu wa jimbo la California, yamekosolewa vikali na wajumbe wa Bunge la Kongresi.
Aghalabu ya wajumbe wa Kongresi wanaamini kuwa matamshi hayo yasiyokubalika hata kidogo ya Trump, yanaonyesha wazi kuwa hawajibiki na ni mchochezi.
Matamshi hayo ya Trump ya kuwavunjia heshima na kuwadhalilisha wahajiri yameandamana na hatua za kivitendo za kuwatenganisha watoto wahajiri na wazazi wao.
Hali kadhalika Trump amewawekea Waislamu vizingiti kuingia Marekani sambamba na hatua zingine nyingi za kibaguzi. Hatua hizo za Trump zinalenga kuwashinikiza wahajiri na wahamiaji ili kuwazuia wasiingie Marekani.
Matamshi ya kibaguzi ya rais wa Marekani ni chanzo cha wasiwasi na hofu katika jamii ya Marekani hasa miongoni mwa wasomi nchini humo ambao wanaamini kuwa matamshi hayo yasiyofaa hata kidogo yataharibu itibari iliyobakia ya nchi hiyo duniani.
Rupert Colville, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa anasema matamshi ya Trump ni ya kushtua na ya kuaibisha.
Ikulu ya White House na hata Donald Trump mwenyewe wamejaribu kukanusha matamshi hayo ya kibaguzi, lakini ukweli usioweza kupingika ni huu kuwa, ubaguzi wa rangi ni sehemu ya utambulisho wa wazi wa utawala wa Rais Trump na Ikulu ya White House.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewafuta kazi zaidi ya mahakimu 250 kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya ufisadi.
Waziri wa Sheria Alexis Thambwe
Mwamba amesema kuwa, mahakimu hao wamefutwa kazi kwa sababu za ufisadi
na wengine kutokuwa na elimu ya taaluma hiyo.
Waziri thambwe amebainisha kuwa, hatua
hii imechukuliwa ili kuwazuia watu waliokuwa wakiingia katika idara ya
mahakama wakiwa na lengo la kujipatia fedha badala ya kuwatumikia raia
wa nchi hiyo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, idadi
kamili ya mahakimu waliofutwa kazi na serikali ni 256 na kwamba, sababu
kuu ni majaji hao kujihusisha na vitendo vya kupokea rushwa, kutokuwa na
elimu ya taaluma hiyo na kundi la tatu limestaafishwa.
Hii sio mara ya kwanza kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo Kinshasa kuwachukulia hatua maafisa wa juu wa idara ya
Mahakama. Mwaka 2009, Rais Joseph Kabila aliwafuta kazi majaji 96 baada
ya kubainika kuwa walikuwa wakijihusha na vitendo vya ufisadi.
Hatua hiyo ya kufutwa kazi majaji hao
inakuja kukiwa kumesalia miezi 7 kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu katika
nchi hiyo inayokabiliwa na changamoto kubwa ya usalama.
Uchaguzi huo uliokuwa ufanyike mwishoni
mwa mwaka jana ulisogezwa mbele na sasa unatarajiwa kufanyika Desemba
23, mwaka huu ili kumpata mrithi wa Rais Joseph Kabila, ambaye muhula
wake wa uongozi ulimalizika Desemba 20, 2016.
Magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria wamewateka watoto zaidi ya 1,000 tokea mwaka 2013.
Hayo
yamedokezwa katika ripoti mpya ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Watoto,
UNICEF ambayo imetolewa kwa munasaba wa kutekwa wasichana 276 wa shule
katika mji wa Chibok kaskazini mashariki mwa Nigeria. Wasichana hao
walitekwa na magaidi wa kundi hilo la Kiwahhabi la Boko Haram.
Mkuu
wa UNICEF nchini Nigeria Mohamed Malick Fall amesema watoto katika eneo
la kaskazini mashariki mwa Nigeria wanaendelea kukabiliwa na
mashambulizi ambayo yanashtua sana. UNICEF imesajili kesi zaidi ya 1,000
za watoto kutekwa nyara lakini imesema idadi hiyo huenda ikawa kubwa
zaidi. Aidha shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema limemhoji
msichana aliyewahi kutekwa na Boko Haram ambaye sasa ana umri wa miaka
17 ambaye amesema alinajisiwa na wapiganaji wa kundi hilo. Anasema
alipata mimba baada ya tukio hilo la kusikitisha na sasa anakabiliwa na
matatizo mengi katika kambi ya wakimbizi huku akikejeliwa kuwa yeye ni
'mke wa wapiganaji wa Boko Haram'.
Katika
usiku wa Aprili 14 kuamkia 15, magaidi wa Boko Haram waliwateka nyara
wasichana 276 ambao wengi wameshaachiliwa lakini 100 bado hawajulikani
waliko na kuna wasi wasi kuwa baadhi wameshafariki huku baadhi wakiwa
wameamua kubakia huko walikotekwa nyara.
UNICEF inasema tokea uanze uasi wa magaidi wa Boko Haram nchini
Nigeria, hadi sasa waalimu zaidi ya 2,295 wameuawa na shule 1,400
kubomolewa.
Neno
Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za
Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini
Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine
zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na
ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile
Cameroon, Niger na Chad.
Boko
Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo
kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu,
limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba
na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.
DRC yasusia mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kukusanya fedha za kuwasaidia raia wa nchi hiyo
Mkutano maalumu uliotishwa na Umoja wa
Mataifa umeanza leo mjini Geneva Uswisi kwa kuchangisha fedha za
kukabiliana na janga la kibinaadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo huku serikali ya Kinshasa ikiususia mkutano huo.
Mashirika ya misaada yanasema kuwa, zaidi ya watu milioni 5
wamelazimika kuyakimbia makazi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia yya
Congo kwa sababu ya mapigano katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Aidha mkutano huo wa wafadhili umeanza leo huku takwimu za Umoja wa
Mataifa zikionesha kwamba, watu milioni 13 wanahitaji msaada huku
thuluthi moja kati yao wakiwa ni wakimbizi wa ndani ambao wanahitaji
msaada wa dharura wa kibinadamu mwaka huu.
Wafadhili hao wa kimataifa wanatafuta kiasi cha dola bilioni 1.7
kuwasaidia watu hao wanaohitaji dawa, chakula na makazi mazuri.
Hata hivyo, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesusia
mkutano huo, ikiyashutumu mashirika ya kiraia kwa kutoa takwimu za uongo
na kulichafulia jina taifa hilo.
Uamuzi huo wa serikali ya Kinshasa wa kususia mkutano huo
umekosolewa, huku baadhi ya wakosoaji wakisema kwamba, serikali yya
Kinshasa ingeshiriki tu katika mkutano huo ili kuwashajiisha wafadhili
watoe misaada kwani wanaoumia ni raia.
Hayo yanajiri katika hali ya ambayo, hivi karibuni Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa lilionya kuwa, hali ya kibinadamu nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo imeendelea kuwa mbaya na imefikia hatua ya kuwa
janga kwenye baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, huku mamilioni ya watu
wakikabiliwa na njaa.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimatataifa ya
Ahlul-Beit (AS) amesisitiza kuwa, utawala wa Aal Saud hauna nafasi
yoyote si ya kielimu wala uungaji mkono wa wananchi na kwamba, akthari
ya wanazuoni wa Kiislamu wanawapinga Mawahabi wa Saudi Arabia.
Ayatullah Muhammad Hassan Akhtari
amesema hayo akiwa nchini Syria na kubainisha kwamba, Maulama waliowengi
wa Kiislamu na mataifa ya Kiislamu wanachukia Uwahabi ulioletwa na Aal
Saud.
Ayatullah Akhtari ameongeza kuwa,
aidiolojia ya uchupaji mipaka ya Uwahabi ambayo inaenezwa na kuungwa
mkono na Saudi Arabia imepelekea kutokea magaidi ambao wamekuwa
wakifanya mashambulio ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.
Katibu Mkuu wa Jumuiya yay Kimataifa ya
Ahlul-Beit (AS) amesema Saudia inataka kulinda nafasi yake kupitia
kuzusha hitilafu na mifarakano pamoja na kutekeleza mauaji dhidi ya raia
wasio na hatia.
Aidha ameashiria juhudi za utawala wa Saudi Arabia za kutaka kuwa na
uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kusema kuwa, hatua
hiyo ya utawala wa Riyadh inalenga kuulinda na kuuhifadhi utawala huo,
hata hivyo jambo hilo linalaaniwa na Waislamu ulimwenguni.
Kadhalika Katibu Mkuu wa Jumuiya yay
Kimataifa ya Ahlul-Beit (AS) amesema kuwa, Saudia imeamua kuuunga mkono
utawala dhalimu wa Israel ili kuifurahisha Marekani.
Ayatullah Akhtari ameashiria pia kwamba,
watawala wa Saudia wamebomoa athari nyingi za Kiislamu katika miji
mitakatifu ya Makka na Madina na kuongeza kwamba, wanachofuatilia Aal
Saud ni kuzusha fitina na mifarakano miongoni mwa Waislamu.
Wanariadha 13 wa Afrika walioenda kushiriki
Michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Australia wametoweka katika
mazingira ya kutatanisha.
David Grevemberg, Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Michezo
ya Jumuiya ya Madola amewaambia waandishi wa habari leo Alkhamisi
mjini Gold Coast kunakofanyika mashindano hayo kuwa: "Wanariadha wengine
watano raia wa Rwanda, Uganda na Sierra Leone wametoweka na kwenda
kusikojulikana."
Ameongeza kuwa, hii ni baada ya wanariadha wengine wanane kutoka
Cameroon kutoweka hapo awali, na sasa idadi hiyo ya wanaichezo wa
Kiafrika waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha nchini humo
imefikia 13.
Serikali ya Australia imetoa viza kwa wanamichezo wanaoshiriki katika
michezo hiyo, kuendelea kuwa nchini humo hadi tarehe 15 mwezi Mei.
Peter Dutton, Waziri wa Masuala ya Ndani ya Australia ameonya kuwa,
mwanariadha yeyote atakayebaki nchini humo kinyume cha sheria baada ya
muda wake wa viza kumalizika, atafurushwa nchini humo kwa nguvu.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, mwaka 2000 wakati wa mashindano
mengine ya Jumuiya ya Madola jijini Sydney, wanaridha zaidi ya 100
waliendelea kuishi katika jiji hilo hata baada ya kumalizika kwa michezo
hiyo.
Kremlin yajibu Twitter ya Trump: Makombora erevu yanapaswa kuelekezwa kwa magaidi, si kwa serikali halali
Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin amesema Moscow Russia haishiriki katika udiplomasia wa Twitter.
Dimitri
Peskov ameyasema hayo akijibu ujumbe ulioandikwa na Rais Donald Trump
wa Marekani katika mtandao wa kijamii wa Twitter ambaye ameitahadharisha
Russia kwamba isubiri makombora ya Marekani huko Syria.
Peskov
amesema kuwa, Russia inaunga mkono hatua madhubuti na inaamini kuwa ni
muhimu kujiepusha na hatua yoyote inayoweza kuchafua zaidi hali iliyopo
hivi sasa.
Mapema
leo Rais Donald Trump wa Marekani aliimbia Russia kupitia mtandao wa
Twitter kwamba ijitayarishe kwa mashambulizi ya makombora "mazuri, mapya
na erevu" huko Syria. Marekani inadai serikali ya Syria imetumia silaha
za gesi ya sumu katika eneo la Douma huko Ghuta Mashariki, suala
linalokadhibishwa na Syria na Russia.
Msemaji
wa Wizara ya Mashauri ya kigeni ya Russia, Maria Zakharova pia amejibu
matamshi hayo akisema: Mashambulizi erevu yanapaswa kuelekezwa kwa
magaidi ni si kwa serikali halali ya Syria.
Russia pia imesema kuwa itayatungua makombora yote ya Marekani
yatakayopigwa kueleka Syria na kwamba itapiga mahala yatakakotokea.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
(Arab League) amelaani jinai za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni dhidi
ya raia wa Palestina.
Ahmad Abul Ghait amelaani jinai za
utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza na kulitaka Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake katika kuwalinda
raia wa Palestina mbele ya jinai za utawala wa Israel.
Mahmoud Afifi, msemaji wa Katibu Mkuu wa Arab League pia jana
alitahadharisha kuhusu kuendelea jinai hizo za utawala wa Kizayuni huko
Ghaza na kueleza kuwa hali ya mambo katika eneo hilo inahitajia
uingiliaji wa jamii ya kimataifa. Afifi alisisitiza kuwa wale wote
waliohusika na jinai dhidi ya raia wa Palestina huko Ghaza inapasa
wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Maelfu ya Wapalestina tarehe 30 mwezi
uliopita wa Machi walifanya maandamano ya amani katika maadhimisho ya
mwaka wa 42 wa "Siku ya Ardhi" kuelekea katika mpaka wa Ghaza na ardhi
za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu; ambapo waandamanaji hao
walikabiliwa na hujuma na mashambulizi ya utawala wa Israel. Katika siku
hiyo ya maandamano hayo ya amani chini ya anuani ya "Haki ya Kurejea",
Wapalestina 17 waliuliwa shahidi na wengine zaidi ya 1400 walijeruhiwa.
Tangu siku hiyo hadi sasa, Wapalestina wasiopungua 29 wameshauliwa
shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel na wengine zaidi ya
3000 wamejeruhiwa. Nchi nyingi na vile vile taasisi za kimataifa
zimelaani jinai hizo za Wazayuni.
Spika wa Bunge la Federali la Somalia,
Mohamed Sheikh Osman Jawari, hatimaye amejiuzulu baada ya nchi hiyo ye
Pembe ya Afrika kushuhudia taharuki na mgogoro mkubwa wa kisiasa kwa
wiki kadhaa.
Dahir Amin Jesow, mmoja wa wabunge ameliambia shirika la habari
la Reuters kuwa, "Asubuhi ya leo tulikuwa tunajiandaa kujadili hoja ya
kumuondoa madarakani Spika, mara ghafla Naibu Spika akaja na barua ya
kujiuzulu Spika huyo na kuisoma mbele yetu. Tumepongeza hatua hiyo ya
kujiuzulu ambayo inakubalika kikatiba, na tunatumai huu ndio mwisho wa
mzozo wa kisiasa nchini."
Wiki iliyopita, Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa
Somalia alisimamisha kikao kingine cha Bunge kilichokusudia kujadili
hoja hiyo ya kumuengua madarakani Spika wa bunge hilo.
Somalia imeshuhudia malumbano makali baina ya Waziri Mkuu wa nchi
hiyo Hassan Ali Khaire pamoja na kundi la wabunge wanaomuunga mkono kwa
upande mmoja, na Spika wa Bunge la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa
upande mwingine.
Mgogoro huo ulianza mapema mwezi jana, baada ya wabunge zaidi ya
100 wanaoegemea upande wa Waziri Mkuu, kuwasilisha hoja bungeni ya
kutaka kuenguliwa madarakani Spika wa bunge, kwa madai kuwa amekuwa
kizingiti kwenye shughuli za bunge hilo.
Mohamed Osman Jawari, Spika wa Bunge la Somalia anatuhumiwa na
wabunge kuwa anatumia vibaya madaraka yake na kuzuia kufanyiwa
marekebisho katiba ya nchi hiyo.
Rais wa zamani wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amewasili katika jela la Curibita kuanza kutumikia kifungo cha miaka 12 jela.
Hatua hiyo ya kujisalimisha kwa polisi ameichukua baada ya mahakama
siku ya Ijumaa kumhukumu kwa mashitaka ya ufisadi. Matangazo ya moja kwa
moja ya vituo vya televisheni vya Brazil yameonesha akiwasili kwa
helikopta katika makao makuu ya polisi katika mji wa Curibita ulioko
kusini mwa Brazil.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 72 aliondoka Sao Paoli akiwa
amezingirwa na walinzi kwenye jengo la muungano wa wafuaji vyuma mjini
humo. Alipenya katikati ya wafuasi wake waliokuwa wanamzuia asiondoke na
kuingia katika gari la polisi. Anasisitiza kuwa mashitaka dhidi yake
yalichochewa kisiasa. Lula alikutwa na hatia ya kupokea rushwa kutoka
kwenye kampuni kubwa ya ujenzi, ili iweze kupata mikataba ya serikali.
Umoja wa Mataifa umesema Myanmar haipo tayari
kuwapokea malaki ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya wanaoishi kambini
katika nchi jirani ya Bangladesh.
Ursula Mueller, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika
Masuala ya Kibinadamu ameyasema hayo baada ya kufanya ziara ya siku sita
nchini Myanmar na kubainisha kuwa, mazingira yalivyo hivi sasa nchini
humo hayaruhusu kurejea nyumbani wakimbizi wa Rohingya.
Amesema, "Kutokokana na kile nilichokishuhudia binafsi, hali mbaya ya
kiafya, ukosefu wa dhamana ya usalama na kuendelea kufurushwa kwa
wakimbizi wengine kutoka mkoani Rakhine ni miongoni mwa mambo
yanayoonyesha kuwa Myanmar haijajiandaa kuwapokea Warohingya hao walioko
Bangladesh.
Mwezi uliopita, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa
ilitahadharisha kuhusiana na kuendelea mauaji ya kizazi yanayofanywa na
serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa
nchi hiyo, huku wakimbizi hao wakisisitiza watarejea nchini Myanmar kwa
masharti mawili; mosi, wadhaminiwe usalama wao na pili wapewe uraia.
Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar tangu mwezi
Agosti mwaka jana katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi, yamepelekea
zaidi ya Waislamu laki saba kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya
Bangladesh.
Kwa mara nyingine, jeshi la Yemen kwa
kushirikiana na Harakati ya Kiislamu ya Answarullah, limeshambulia kwa
kombora ghala la kuhifadhia mafuta la Shirika kubwa la Mafuta nchini
Saudia Aramco katika mji wa Jizan, kusini magharibi mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la
Yemen imesema kuwa, kombora lililotumika kushambulia ghala hilo la
mafuta ni aina ya Badr-1 na kwamba lilifyatuliwa jana usiku. Wakati huo
huo duru za serikali ya Saudia zimedai kwamba, ngao ya kuzuia makombora
ya nchi hiyo lilifyatua kombora na kuliharibu kombora hilo la jeshi la
Yemen kabla ya kufika eneo lengwa.
Hili ni shambulio la pili la kombora la
balestiki kufanywa na jeshi la Yemen na Harakati ya Answarullah dhidi
ya shirika la mafuta la Saudia katika kipindi cha wiki moja. Alkhamisi
iliyopita pia, jeshi la Yemen lililishambulia kwa kombora la balestiki
shirika kubwa la uzalishaji mafuta la Saudia ambapo wakati viongozi wa
Riyadh wakidai pia kwamba kombora hilo lilizuiliwa, baadhi ya duru
zilisema kuwa, kombora hilo lilifika eneo lengwa. Kadhalika viongozi wa
Saudia walidai kwamba tarehe 25 mwezi jana, jumla ya makombora saba
yalivurumishwa kutoka nchini Yemen ambapo matatu kati yake yalianguka
katika mji wa Riyadh.
Mashambulizi ya makombora ya harakati ya
Answarullah na jeshi la Yemen yanajiri huku hujuma za Saudia kwa
kushirikiana na nchi kadhaa za Kiarabu na Magharibi dhidi ya Yemen
zikiwa zimeingia mwaka wa nne. Aidha uwezo wa makombora ya harakati hiyo
unashuhudiwa huku Yemen ikiwa imewekewa mzingiro wa kila upande na nchi
wavamizi.