Umoja wa Mataifa umesema Myanmar haipo tayari
kuwapokea malaki ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya wanaoishi kambini
katika nchi jirani ya Bangladesh.
Ursula Mueller, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika
Masuala ya Kibinadamu ameyasema hayo baada ya kufanya ziara ya siku sita
nchini Myanmar na kubainisha kuwa, mazingira yalivyo hivi sasa nchini
humo hayaruhusu kurejea nyumbani wakimbizi wa Rohingya.
Amesema, "Kutokokana na kile nilichokishuhudia binafsi, hali mbaya ya
kiafya, ukosefu wa dhamana ya usalama na kuendelea kufurushwa kwa
wakimbizi wengine kutoka mkoani Rakhine ni miongoni mwa mambo
yanayoonyesha kuwa Myanmar haijajiandaa kuwapokea Warohingya hao walioko
Bangladesh.
Mwezi uliopita, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa
ilitahadharisha kuhusiana na kuendelea mauaji ya kizazi yanayofanywa na
serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa
nchi hiyo, huku wakimbizi hao wakisisitiza watarejea nchini Myanmar kwa
masharti mawili; mosi, wadhaminiwe usalama wao na pili wapewe uraia.
Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar tangu mwezi
Agosti mwaka jana katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi, yamepelekea
zaidi ya Waislamu laki saba kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya
Bangladesh.
No comments:
Post a Comment