Tuesday, June 12, 2018

WITO WA MSHIKAMANO WA NCHI ZA ULAYA KATIKA KUKUBALIANA NA MAREKANI

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amebainisha masiktiko yake baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kukataa kuidhinisha taarifa ya mwisho ya kikao cha viongozi wa nchi tajiri kiviwanda G7 ambacho kilimalizika juzi huko Quebec, nchini Canada. Merkel amebainisha wazi kuwa nchi za Ulaya hazipaswi kuitegemea tena Marekani.
Naye Heiko Maas Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesisitiza kuwa, jibu la  Ulaya kuhusu uamuzi huo wa Trump linapaswa kuwa ni mshikamano na ukuruba zaidi katika Umoja wa Ulaya.
Mass ameongeza kuwa uamuzi wa Trump wa kutoafiki taarifa ya mwisho ya kikao cha G7 haukuzishangaza sana nchi shiriki kwani Trump amekiuka mapatano mengine muhimu ya utunzaji mazingira  na mapatano ya nyuklia ya Iran.
Baada ya mkutano wa viongozi wa kundi la G7, kumedhihirika hitilafu kubwa na za wazi baina ya Rais Trump na viongozi wa Canada, Ufaransa na Ujerumani. Trump aliondoka mapema kabla ya kikao hicho kumalizika kama ishara ya kubainisha kuchukizwa kwake na tamko la Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na kusema hataunga mkono taarifa ya mwisho ya kikao hicho. Uamuzi huo wa Trump umetajwa kuwa ni pigo kubwa kwa kundi la G7 ambalo linajumuisha  Marekani, Canada, Ujerumani, Uingereza,Ufaransa, Italia na Japan.

Trump amejiondoa katika mapatano ya kulinda mazingira duniani ya Paris 

Hatua hiyo ya Trump itatoa pigo kubwa kwa ushirikiano wa pande mbili za Bahari ya Atlantiki na pia ni pigo kubwa kwa uhusiano wa kistratijia wa Canadan na Marekani. Kwa hatua yake hiyo, Trump analenga kung'oa mizizi ya uhusiano na mshikamano wa miongo kadhaa wa kiuchumi, kibiashara, na kiusalama baina ya Marekani na Ulaya. Wakuu wa Ulaya wanajaribu kuzuia hali ya mambo kuwa mbaya zaidi na wanasema hatua ya Trump kutosaini taarifa ya mwisho haimaanishi kila kitu kimekwisha. Kuhusiana na hili, Angela Merkel amesema: "Hatua ya Trump kutangaza kuwa hatatia saini taarifa ya mwisho ya G7 kupitia Twitter ni jambo la kusikitisha. Ameongeza kuwa, 'kikao cha viongozi wa G7 huko Canada hakikuwa mwisho wa ushirikiano wa Ulaya na Marekani lakini akaongeza kuwa, nchi za Ulaya hazipaswi kuitegemea tena Marekani na zinapaswa zenyewe zijiamulie  hatima yao.'
Ingawa suala la Marekani kujiondoa G7 halijapewa uzito mkubwa lakini kwa kuzingatia utendaji kazi wa Trump katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu wa urais wake, nchi zingine sita za kundi la G7 hazitashangaa iwapo Trump ataendeleza mwenendo wake huo wa kupuuza na kubatilisha mikataba ya kimataifa, na hivyo aamue kujiondoa katika kundi hilo. Kwa hivyo nchi hizo sita zinajitayarisha kwa hali kama hiyo.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anasema hivi kuhusu suala hilo:"Pengine Trump hajali iwapo atatengwa lakini hata tukibadilika na kuwa kundi la  G6 bado tutakuwa nguvu kubwa. Iwapo Trump ataamua kuiondoa Marekani katika nafasi yake duniani, jambo hilo litakuwa na matokeo hasi kwa uchumi na hadhi ya Marekani duniani. Trump anafahamu hili."

Trump amejiondoa katika maptano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA

Mtazamo wa Trump kuhusu masuala ambayo yamepelekea kuibuka hitilafu baina ya Marekani na Ulaya ni jimbo linaloonyesha kuwa hana nia ya kulegeza msimamo wake bali hata ametoa vitisho kwa kwa nchi za Ulaya na Canada hasa katika masuala ya kibiashara. Trump ameongeza kwa kiwango kikubwa ushuru wa bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka Ulaya, Canada na Mexico hasa bidhaa za chuma.
Hatua hizo za Trump zimepelekea kuongezeka hitilafu kubwa baina ya Marekani na nchi hizo na kuwepo hatari ya kuibuka vita vya kibiashara kati ya Marekani na nchi hizo. Hali kadhalika nchi za Ulaya pia zimekasirishwa na hatua ya Trump ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA na mapatano mengine muhimu ya mazingira maarufu kama Mapatano ya Tabianchi ya Paris.
Kwa mtazamo wa nchi muhimu katika Umoja wa Ulaya, si tu kuwa sera za Trump zitaidhuru dunia bali zitapelekea kutengwa zaidi Marekani katika uga wa kimataifa.

No comments:

Post a Comment