Kwa mara nyingine, jeshi la Yemen kwa
kushirikiana na Harakati ya Kiislamu ya Answarullah, limeshambulia kwa
kombora ghala la kuhifadhia mafuta la Shirika kubwa la Mafuta nchini
Saudia Aramco katika mji wa Jizan, kusini magharibi mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la
Yemen imesema kuwa, kombora lililotumika kushambulia ghala hilo la
mafuta ni aina ya Badr-1 na kwamba lilifyatuliwa jana usiku. Wakati huo
huo duru za serikali ya Saudia zimedai kwamba, ngao ya kuzuia makombora
ya nchi hiyo lilifyatua kombora na kuliharibu kombora hilo la jeshi la
Yemen kabla ya kufika eneo lengwa.
Hili ni shambulio la pili la kombora la
balestiki kufanywa na jeshi la Yemen na Harakati ya Answarullah dhidi
ya shirika la mafuta la Saudia katika kipindi cha wiki moja. Alkhamisi
iliyopita pia, jeshi la Yemen lililishambulia kwa kombora la balestiki
shirika kubwa la uzalishaji mafuta la Saudia ambapo wakati viongozi wa
Riyadh wakidai pia kwamba kombora hilo lilizuiliwa, baadhi ya duru
zilisema kuwa, kombora hilo lilifika eneo lengwa. Kadhalika viongozi wa
Saudia walidai kwamba tarehe 25 mwezi jana, jumla ya makombora saba
yalivurumishwa kutoka nchini Yemen ambapo matatu kati yake yalianguka
katika mji wa Riyadh.
Mashambulizi ya makombora ya harakati ya
Answarullah na jeshi la Yemen yanajiri huku hujuma za Saudia kwa
kushirikiana na nchi kadhaa za Kiarabu na Magharibi dhidi ya Yemen
zikiwa zimeingia mwaka wa nne. Aidha uwezo wa makombora ya harakati hiyo
unashuhudiwa huku Yemen ikiwa imewekewa mzingiro wa kila upande na nchi
wavamizi.
No comments:
Post a Comment